
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Juma Nkamia akitoa hotuba wakati wa uzinduzi wa akaunti maalum za
wanachama wa Simba na Yanga iliyoandaliwa na Benki ya Posta Tanzania (TPB)
kwenye ukumbi wa Hyatt Regency jijini Dar es Salaam leo.
Na Bertha Lumala
Imechapishwa Mei 30, 2014, saa 12: 15 jioni
SERIKALI imewataka viongozi
wa klabu kongwe nchini Simba na Yanga kuhakikisha wanamaliza migogoro
inayoendelea kwa sasa katika klabu hizo ili kuleta utulivu katika tasnia ya
michezo nchini.
Juma Nkamia, Naibu Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, katika hotuba yake aliyoitoa wakati hafla ya uzinduzi wa
akaunti maalum kwa ajili ya mashabiki na wanachama wa Simba na Yanga kwenye
Hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam muda mfupi uliopita, ameonya tabia za
fujo na uhuni unaofanywa na baadhi ya wapenzi wa klabu hizo na kuwaagiza
viongozi kuhakikisha wanarejesha utulivu.
“Kati ya vitu vinavyokera kwenye tasnia ya
michezo ni migogoro ya klabu. Na migogoro hii haifanywi na wachezaji bali
viongozi wa klabu kwa manufaa yao binafsi,” amesema Nkamia.
“Kuna desturi imejengeka kwamba kuwa kiongozi
wa Simba au Yanga kwa sasa ni dili. Simba sasa wameanza vurugu katika mchakato
wa uchaguzi wao. Kwa niaba ya serikali, ninawaomba viongozi wahakikishe
wanarejesha utulivu kipindi hiki cha uchaguzi.
“Simba na Yanga ni timu kongwe nchini na
zimekuwa zikitoa wachezaji wengi wa timu ya taifa. Kuibuka kwa migogoro na fujo
ndani ya klabu hizo kuna athari hata kwa timu ya taifa na soka la Tanzania kwa
ujumla.”
Nkamia pia ameipongeza Benki ya Posta Tanzania
(TPB) kwa kuanzisha akaunti maalum kwa ajili ya mashabiki wa Simba na Yanga kwa
kuwa anaamini maamuzi hayo ni hatua kubwa katika kuzisaidia klabu hizo kimapato
na kurahisha kazi ya kutambua idadi ya wanachama wa klabu hizo na michango yao.
Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa TPB, Sabasaba
Moshingi amesema lengo kuu la kuanzisha akaunti hizo ni kuziwezesha klabu hizo
mbili kuongeza kipato na kurahisisha kazi ya viongozi wa klabu hiyo kuwafahamu
wanachama walio hai na mashabiki wao.
Amesema kadi hizo zitawawezesha wanachama
kuingia katika mikutano yote ya klabu hizo na kwamba zitakuwa za aina mbili; za
wanachama wa kawaida na wanachama wakubwa (VIP).
“Simba na Yanga ni klabu kongwe nchini kwa
maana zipo tangu miaka ya 1930 lakini bado zinakabiliwa na changamoto ya
kiuchumi. Tumeona tuanzishe utaratibu huu kujitegemea kifedha kupitia michango
ya wanachama wake,” amesema Moshingi.
Ismail Aden Rage, Rais wa Simba, amesema
kuanzishwa kwa akaunti hizo kutaisaidia klabu yake kujiendesha pasipo kutegemea
wanachama wake wenye majina makubwa.
“TPB kwa kuanzisha akaunti hii watatusaidia
kuondoka na utaratibu wa kutegemea fedha za watu wanaojigeuza miunguwatu ili
waabudiwe,” amesema Rage.
“Kama nilivyoahidi katika uongozi wangu,
nitaachia Simba uwanja. Juni 21 nitakadhiwa uwanja wenye magoli na wenzetu wa
TPB wametuahidi kutujengea hosteli ili wachezaji wetu waondokane na utaratibu
wa kuweka kambi kwenye hoteli.
“Kadi hizi za uanachama za Simba zinazotolewa
na TPB zitarahisha usajili wa wanacha wetu kwa sababu watajisajili kwa siku
moja na kupewa kadi yao muda huo huo. Hakuna mkombozi wa Simba kwa sasa zaidi ya
Benki ya Posta Tanzania.” amesema zaidi Rage.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga,
amesema uongozi uliopo kati yao na Simba ni wa uwanjani tu na wataendelea
kushirikiana katika masuala mengine yote ya nje ya uwanja likiwamo la
kujikwamua kiuchumi.
Baadhi ya viongozi wa michezo waliohudhuria
hafla hiyo ni pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Leonard
Thadeo, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Simba, Michael Wambura, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu na Katibu wa Simba,
Ezekiel Kamwaga.
0 comments:
Post a Comment