
…………………………………………………
Nianze kwa kuwashukuru sana wasomaji wa www.fullshangweblog.com nawww.bkmtata.blogspot.com (MPENJA BLOG). Hakika mmekuwa karibu yetu na kuendelea kutuamini zaidi na zaidi.
Timu nzima ya mitandao hii miwili, tunayo furaha kubwa kutokana na imani yenu juu yetu.
Kwa niaba ya mkurugenzi wangu wa Flavour Media Company LTD, Mmiliki wa Tovuti hii yaFULLSHANGWEBLOG, Bwana John Bukuku, tunawaahidi kufanya kazi nzuri kwa faida yetu WOTE.
Simu zenu, jumbe zenu za simu zimekuwa msaada wa kutuweka kwenye njia sahihi. Mmekuwa wepesi wa kutushauri na kutukosoa pale tunapofanya makosa.
Tunakubaliana na ukosoaji wenu, bila kusahau pongezi zenu pale tunapofanya vizuri. Mungu awabariki sana.
Katika salamu zangu siku ya leo, napenda kuwashirikisha jambo lifuatalo;
Asilimia kubwa ya watu duniani wanaamini uwepo wa Mungu, Muumba mbingu na nchi.
Hata mimi ni mmoja kati ya watu hao. Namuamini Mwenyezi Mungu aketie mahali palipoinuka. Hakika amekuwa msaada mkubwa kwangu kuniweka hapa nilipo.
Katika kusikiliza muziki, kuna dada mmoja ametunga wimbo mmoja ambao ndani yake kuna maneno yameandikwa hivi “Mungu hugawa riziki kwa mafungu, tuvumilie muda wetu haujafika”. Maneno hayo alikuwa anamwambia mpenzi wake katika huo wimbo.
Ni maneno mafupi sana, lakini nikatafakari kwa muda mrefu na kubaini yana ukweli ndani yake kwa sisi tunaoamini katika Mungu.
Hapa nasemea kumuamini Mungu kwa imani zote. Sijakusudia kusemea imani moja.
Nimewasikie watu wengi wakiwa wamekata tamaa na kuona hawawezi tena kuinuka na kufikia malengo yao.
Utawasikia wakilaumu sana na wakati mwingine kumlaamu hata Mungu kwa madai kuwa amewasahau na kuwaacha katika maisha ya dhiki.
Lakini nimejifunza kuwa kila jambo lina wakati wake. Kama imani yako imejengwa katika Mungu, basi kuna siku itafungua njia zake.
Niliseme hili mapema kabisa. Nadhani ni dhambi kubwa kutofanya kazi kwa bidii na ukategemea muujiza kutoka kwa Mungu.
Hata maandiko yako wazi kuwa asiyefanya kazi na asile. Lazima uchangamkie maisha yako kwa kufanya kazi kwa kujituma zaidi.
Nafahamu kuwa wengi wetu tunataka mafanikio ya haraka, na pale mambo yanapokwenda ndivyo sivyo, tunakimbilia kulaamu na kunung`unika.
Nimejifunza kuwa hata ulaumu vipi, Mungu atabaki kuwa Mungu na hutoa kwa wakati wake.
Kamwe! hatakuweka mkia kama unamwamini kwa roho na kweli. Fungu lako likifika atakufanya kuwa kichwa.
Ipo haja kubwa ya kuendelea kupigania maisha ya hapa duniani, lakini usisahau kumuomba mwenyezi Mungu katika harakati zako.
Cha msingi uwe na bidii katika kazi zako. Fanya mambo yako kwa ufanisi mkubwa, hakika utafikia malengo yako.
Usijaribu kuiga maisha ya mtu, jenga misingi yako kwa kuiga watu waliokutangulia endapo utagundua wamefanya yale unayotarajia.
Katika kazi zako kuwa na uvumilivu. Haitokei ukalala masikini ukaamka tajari. Mafanikio yana njia zake.
Usipende njia ya mkato, huwa ni hatari sana. Kubali kukosolewa na kujifunza kwa haraka.
Najua umesikia vijana wengi wakikamatwa katika utapeli, wizi, dawa za kulevya n.k. Kinachowasukuma kufanya haya ni kupenda njia ya mkato kutafuta mafanikio.
Pita njia sahihi, michepuo sio dili. Ukibaki njia kuu na kufanya kazi kwa bidii utapata mafanikio.
Usiwe na haraka. Vumilia tu itafika wakati juhudi zako zitazaa matunda.
Wakati unafanya haya yote, jijenge katika misingi ya kuwa na heshima, busara na hekima kwa watu walio chini yako na juu yako.
Heshima yako itasaidia kuvuna Baraka na kupokea ushauri kwa watu wote. Hii itakuwa silaha yako ya ushindi.
Pia jenga utamaduni wa kutafuta taarifa. Soma kila unachokiona mbele yako. Tafuta taarifa kwa muda wote.
Kinachowatafuna watu wengi ni kukosa taarifa, na huwezi kupata taarifa kama ni mvivu wa kusoma.
Kusoma kunajenga uwezo mkubwa wa kutafakari na kupata njia nyingi za kutafuta mafanikio.
Hakuna uchawi katika mafanikio, bali ni kujituma tu.
Kwa wale wanaoamini uchawi, inawezekana unasaidia kutafuta mafanikio, lakini bado sijafikia hatua ya kuamini hayo.
Lazima tuwe na ujasiri wa kuthubutu, hakika tutaweza.
Nawatakieni kila la heri na mafanikio mema.
Nimeandika haya si kwamba nimefanikiwa wala kusogelea ndoto zangu, bali ni salamu zangu kwenu katika kutiana moyo kwenye safari hii ndefu ya kusaka mafanikio.
Na Baraka Adson Mpenja
0712461976 ua 0764302954
Mhariri Mkuu Mtandao wa www.fullshangweblog.com
Pia mmiliki wa blog ya www.bkmtata.blogspot.com MPENJA BLOG
0 comments:
Post a Comment