
Rais wa TFF, Jamal Malinzi jana alikabidhiwa rasmi ofisi na Rais aliyemaliza muda wake, Leodigar Chila Tenga
Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
BAADA
ya Rais wa zamani wa shirikisho la soka Tanzania, TFF Leodigar Chila
Tenga kukabidhi ofisi hapo jana kwa Rais Mpya, Wadau wa soka nchini
Tanzania hususani wanaopenda maendeleo wametakiwa kumuunga mkono Rais wa
sasa wa TFF, Jamal Emily Malinzi ili kufanikisha ilani yake
iliyosheheni mipango mingi yenye tija kwa mpira wa Tanzania.
Mshambuliaji
wa zamani wa klabu ya Yanga na Taifa Stars, Sekloja Johnson Chambua
ambaye kwa sasa ni kocha wa mpira wa miguu amesema Rais Malinzi ana sera
nzuri za kuendeleza soka la Tanzania, lakini peke yake hataweza kufikia
malengo yake, hivyo wadau wampe sapoti kubwa ili taratibu zake
alizojipangia ziweze kufikiwa.
“Malinzi
ameongelea vizuri mipango yake ya kuendeleza soka la vijana, sera
alizosema ni nzuri, kinachofuata ni utekelezaji wa sera zake. Mara
nyingi tumekuwa tukizungumza sana bila kutekeleza, cha msingi kwa Rais
wetu ni kutekeleza kila alichosema, lakini bado wadau nao wanatakiwa
kuwa karibu naye”. Alisema Chambua.
Chambua
alisema soka la vijana ndio msingi muhimu, hivyo lazima wapenda michezo
kuungana kutekeleza sera zake, ila ni muhimu kwa Malinzi kuhakikisha
suala la makocha linawekewa uzito kama alivyoahidi.
“Kuna
makocha wengi wenye kozi za awali hapa nchini, nimuombe Rais Malinzi
kuwasaidia makocha hawa kujiendeleza ili wawe bora zaidi. Kama unavyojua
nchi hii ni kubwa, tunatakiwa kusambaza makocha kila sehemu ili kuibua
na kuendelea vipaji kwa vijana”. Alishauri Chambua.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa kituo cha vijana cha Morogoro (Morogoro Youth
Soccer Academy), Rajab Kindagule amesema walikuwa na ushirikiano mkubwa
na uongozi wa Tenga, hivyo wanasubiri ushirikiano kama huo au zaidi
kutoka kwa Rais mpya , Jamal Malinzi.
“Sijui
Malinzi anataka mfumo gani, lakini ameongea vizuri katika sera zake,
inaonekana ana nia ya kuendeleza soka la vijana. Tunapanga kuonana naye
ili tumpe pongezi na kumueleza mambo mbalimbali yahusuyo soka”. Alisema
Kindagule.
Kindagule
aliyewaibua wachezaji maarufu na vijana kwa sasa, Shomary Kapombe
aliyeko Ufaransa, Willium Lucian `Gallas` , Edward Christopher waliopo
Simba na wengine wengi aliongeza kuwa ni lazima Malinzi apewe sapoti
kubwa kwani kiukweli ilani yake imezungumzia mambo mengi ya msingi
katika soka la Tanzania.
Naye
kocha wa klabu ya Njombe mji na mjumbe wa kamati ya ufundi ya klabu ya
Simba sc, John William `Del Piero` amemuomba Rais Malinzi kukaa chini na
kamati yake ya utendaji na kujenga ushirikiano mkubwa ili kufanikisha
ilani yake inayoonekana ngumu kulingana na uzito wa mambo aliyoyasema.
Rais
Malinzi ameweka wazi sera zake na kiukweli kagusa maeneo mengi yenye
mapungufu, lakini tukimuacha afanye peke yake na kuendekeza makundi na
tofauti za kiushabiki, basi atashindwa kufanikisha mengi.
“Binafsi
nina imani kubwa na Bwana Malinzi, ni mtu wa mpira, ana uzoefu mkubwa.
Nadhani atashirikiana na viongozi wenzake kufikia malengo”. Alisema
Piero.
Jana
wakati anakabidhiwa ofisi, Rais Malinzi alisema Uongozi wake
unakabiliwa na nyingi ambazo hawezi kuzitaja kwa pamoja, lakini chache
zinazohitaji ufumbuzi wa haraka ni:
Hii ni sehemu ya Hotuba ya Malinzi jana, soma ili utambua nini alichosema:
Mashindano yanayotukabili.
Malinzi
alisema ; “Tunakabiliwa na mashindano mbalimbali ya kimataifa. Mfano ni
mechi ya marudiano ya U/20 wanawake dhidi ya Msumbiji wiki ijayo,
Mitoano ya mashindano ya Afrika wanawake mapema mwakani, Mashindano ya
Chalenji Novemba mwaka huu, na mashindano ya kufuzu AFCON 2015. Yote
haya yanahitaji maandalizi ya haraka”.
Programu ya vijana.
“Ilani
yangu ya uchaguzi ilielezea azma ya Tanzania kuomba uenyeji wa fainali
za vijana za Afrika U/17 mwaka 2019. Jambo hili tutalizungumzia kwenye
kikao chetu cha utendaji leo. Ili tuwe na timu nzuri ya kucheza fainali
hizo tukiwa wenyeji hatuna budi mwaka kesho kuunda timu ya Taifa ya U/12
itakayokua pamoja kuelekea 2019. Programu yetu ya vijana tutakayoiandaa
sharti ijielekeze kwenye ratiba hii.”
Udhamini wa timu za vijana na za wanawake
“Hii
ni changamoto kubwa sana kwa TFF. Timu zetu za Taifa kuanzia zile za
wakubwa hadi za vijana ni brands, na kama ni brands inabidi ziingizwe
sokoni, ziuzwe kwa tunaodhamiria wawe wadhamini wa hizo timu. Kitengo
cha masoko lazima kiimarishwe ili kukabiliana na changamoto hizi.
Mdhamini ni mfanyabiashara, anapotoa pesa kudhamini brand fulani
anategemea matokeo mazuri kwake kwa njia ya kukuza biashara zake. Twende
kwa wadhamini tuwashawishi waone watafaidikia nini (leverage) kwa
kudhamini timu zetu. Tusisubiri waje tuwafuate sisi.”
Uwekezaji
“Jitihada
za haraka lazima zifanyike kuiongezea TFF uwezo wa kiuchumi. Ni muhimu
mtaalam mshauri (consultant) atafutwe atufanyie mchanganuo wa uwekezaji
katika ardhi yetu hii ya Karume ili tuwekeze kitega uchumi kama
ilivyokubaliwa kwenye mkutano mkuu. Aidha bidhaa zenye nembo yetu zianze
kuuzwa kwa utaratibu maalum ili shirikisho lipate haki yake.”
“Kabla
sijamaliza kuzungumza, niongelee suala la fujo viwanjani. Mpira ni
dakika tisini. Katika kipindi hicho uamuzi wa mwamuzi unakuwa ni wa
mwisho. Tusifiche upungufu wa timu zetu kwa kujificha nyuma ya kivuli
cha mwamuzi. Waamuzi wakionekana wamefanya makosa yawe ya makusudi au ya
bahati mbaya vyombo vya kuwahukumu vipo, mahakama ya waamuzi sio
mashabiki. Kitendo cha mashabiki kufanya fujo kabla, wakati na baada ya
mechi ya mpira kamwe hakikubaliki mahali popote duniani. Kanuni za
FIFA, CAF na TFF ziko wazi na adhabu zinajulikana. Moja ya adhabu hizi
ni timu husika kucheza kwenye uwanja mtupu usio na mashabiki kama
ilivyowatokea Al Ahly na Zamalek huko Misri au kucheza nje ya uwanja
wako kama ilivyowatokea Senegal ambao baada ya vurugu Dakar, Senegal
waliamriwa na FIFA mechi zao za nyumbani wachezee nje ya nchi na
wakachagua kuchezea Morocco.”
“Ndugu
zangu yaliyotokea majuzi Mbeya na Dar es salaam wote tumeyasikia na
wengine miongoni mwetu hapa ni mashuhuda. Ninasema iwe mara ya kwanza na
y a mwisho. Kwenye masuala ya kutekeleza mahitaji ya kanuni uongozi
wangu hautaionea haya klabu yoyote, iwe mpya au kongwe kwenye ligi yetu.
Ni jukumu la viongozi wa klabu kudhibiti wanachama na wapenzi wao.
Tabia ya benchi la ufundi kutoa matamshi yanayoweza kuamsha hisia za
mashabiki ni kinyume na taratibu na kanuni ziko wazi kuhusu jambo hili.
Viongozi wa klabu na mabenchi yao ya ufundi wakishindwa kutekeleza
wajibu wao tusilaumiane.”
“Ndugu
zangu ya kufanya ni mengi katika kuiendeleza soka yetu. Tunashukuru
Mungu kuwa uwezo wa kukabiliana na changamoto hizi tunao na tuna ari na
nia ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mpira. Ombi langu kwenu
nyote ninaomba ushirikiano wa wadau wote kuanzia Serikali, Halmashauri,
mashirika ya umma na binafsi na NGO’s, nina imani tukishikamana
tutaifikia ndoto yetu ya kuing’arisha Tanzania kimpira kwenye anga za
dunia.”
0 comments:
Post a Comment