Waziri wa katiba na Sheria , Mhe chikawe
……………………………………………………………………………………………………………….
Kupitia
kipindi cha Wanawake Live kinachorushwa na EATV kila siku ya Jumanne
saa tatu usiku, umma wa Watanzania walipata kufahamu kilichomkuta binti
Emma Roberts. Kwa kukumbusha tu, Emma ni binti aliyefukuzwa shule
kutokana na ujauzito. Ujauzito wa Emma ulikuja baada ya kufanyiwa
kitendo cha ukatili cha ubakwaji. Kwa mdomo wake mwenyewe, Emma
ameelezea hali halisi na kusema kwamba hakupenda huo ndio uwe
mustakabali wake wa maisha kwa kuwa alikuwa na ndoto nyingi sana katika
maisha. Emma hakupenda kubakwa. Tukio hilo limemkosesha nafasi ya kupata
haki yake ya msingi, elimu. Emma katika maelezo yake anasema elimu ndio
ingemsaidia katika maisha yake yeye na mwanae. Akiwa na namba yake ya
mtihani tayari kwa ajili ya kufanya mtihani wa kidato cha nne 2013, Emma
alisubiria kwa hamu majibu ya ombi lake kwa Wizara ya Elimu imruhusu
kufanya mtihani huo. Hata hivyo, Emma hakuweza tena kufanya mtihani kwa
kuwa hakupewa ruhusa ya kufanya hivyo.Kupitia
Wanawake Live, Waziri wa Sheria na Katiba Mhe Mathias Chikawe
amezungumza na kueleza sheria ikoje katika masuala kama haya, na
kumalizia kuwa ‘Hakuna mimba za bahati mbaya’. Maswali ambayo wengi
wanajiuliza ni pamoja na Je, sheria inayotumika kuongoza elimu nchini
Tanzania, inawanufaisha wananchi au ni sheria iliyowekwa kukandamiza
kikundi fulani cha watu? Je, Emma Roberts hakupaswa kupigania haki yake
ya kupata elimu eti kwa sababu Mhe Waziri wa Sheria na Katiba amesema
kwamba ‘Hakuna mimba za bahati mbaya’?
Mara zote jamii imeshuhudia
wasichana wadogo wakifukuzwa shule kutokana na tatizo la mimba, bila
kutazama chanzo cha mwanafunzi huyo kupata hiyo mimba. Pia, wahusika
wakuu wa mimba hizo (wanaume) wengi wamethibitika kuendelea kupeta tu
mtaani bila kuchukuliwa hatua zozote ilhali msichana anakuwa
ameshafukuzwa shule na kunyimwa haki yake ya kimsingi. Muda umefika sasa
wanawake kupigania haki zao dhidi ya sheria kandamizi ambazo
zinawanyima fursa muhimu katika maisha. Pia, mawazo mgando kama ya Mhe.
Chikawe eti ‘hakuna mimba za bahati mbaya’ ni kitu kinachopaswa kupigwa
vita vikali.
SOURCE: http://wanawakelivetv.com/
0 comments:
Post a Comment