Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
VINARA
wa ligi kuu soka Tanzania bara, klabu ya Azam fc wana `Lambalamba`
wamekiri kukabiliwa na mchezo mgumu zaidi dhidi ya Mbeya City siku ya
alhamisi (Novemba 7 mwaka huu) uwanja wa Azam complex, Chamazi, Nje
kidogo ya Dar es salaam.
Afisa
habari wa klabu hiyo, Jafary Idd Maganga amesema katika ligi hakuna
mechi nyepesi na hiyo ndiyo falsafa yao, lakini mchezo ujao dhidi ya
timu wanayofukuzana nayo ni mgumu zaidi kwani vijana hao ni hatari na
wanashindana mwanzo mwisho.
“Tulianza
ligi kwa sare nyingi, watu walitudharau na kusema hatuna lolote, sasa
ni mechi tano tumeshinda mfululizo na tupo kileleni. Lengo letu ni
kuendelea kushikilia usukani, hivyo tunajiandaa kwa nguvu zote
kuhakikisha tunapata ushindi mbele ya Mbeya City, vijana machachari
kabisa”. Alisema Jafary.
Jafary
aliongeza kuwa vijana wao akiwemo Farid Musa, Joseph Kimwaga wamekuwa
wakisaidiwa na wachezaji wakubwa kupata uzoefu na wataendelea kufanya
hivyo kwani Azam fc ni timu pekee hapa Tanzania iliyoanzishwa na kujenga
kituo cha kulelea vijana kwa wakati huo huo.
“Azam
fc ni timu inayoamini soka la vijana, tunajua kuwa vijana hawawezi kuwa
tegemeo, sisi tuna wachezaji wazoefu ambao wanafanya kazi ya kuwaongoza
vijana wetu. Kocha wetu pia amekubali mfumo wetu na tutaendelea hivi
mpaka mwisho”. Alisema Jafary.
Kwa
upande wao Mbeya City kupitia kwa kocha wao mkuu, Juma Mwambusi
wametamba kupambana vikali na Azam fc ambao ni timu bora ili kuvuna
pointi tatu muhimu kwao.
Mwambusi
alisema maandalizi waliyoyafanya kutoka awali ni kwa mechi zote 26 za
ligi kuu soka Tanzania bara, ingawa wanatambua ugumu wa Azam, lakini
wamejiandaa kutafuta ushindi ili kushika usukani kwa mara ya kwanza
tangu kuanza kwa ligi.
“Kwanza
niwapongeze vijana wangu kwa kuendelea kufuata maelekezo yangu,
wanacheza vizuri na ndio maana najiamini ninapoenda kukutana na Azam fc
wakiwa nyumbani. Niwaombe mashabiki wa soka Mbeya, waje kwa wingi
kuishangilia timu yao kwani ipo tayari kwa mapambano”. Alisema Mwambusi.
0 comments:
Post a Comment