
Na Baraka Mpenja
Wakata
miwa wa mashamba ya miwa ya Manungu Turiani mkoani Morogoro, wana
“TamTam “ Mtibwa Sugar wanaofundishwa na kocha mzawa Mecky Mexime
wanatarajiwa kuanza kupiga jalamba la uhakika katikati ya mwezi huu wa
saba ili kujiandaa na mitanange ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu
mpya unaotarajiwa kuanza Agosti 24.
Mwenyekiti
mwenye dhamana ya kuiongoza timu hiyo kubwa nchini Tanzania yenye
historia ya kuzisumbua Simba na Yanga na kutwaa taji miaka ya nyuma,
Jamal Baiser amesema kwa sasa wanafanya mipango ya kusajili wachezaji wa
kuziba nafasi zilizoachwa wazi kufuatia baadhi ya wachezaji kutimka
klabuni hapo.
“Mpaka
sasa hatujasajili wachezaji, lakini mipango yetu ni kusajili wachezaji
wapatao watano, na baada ya kukamilisha taratibu zote, tutawajulisha
mashabiki wetu. Kikubwa ni kwamba, tunahitaji kuwa na timu nzuri zaidi
kuliko misimu mitatu iliyopita”. Alisema Baiser.
Baiser
alisema kwa muda mrefu sasa, Mtibwa sugar haifanyi vizuri sana wala
vibaya sana, lakini kwa msimu ujao wanajiandaa kuwa timu bora zaidi,
huku wakichanganya damu changa na kongwe katika kikosi chao.
Mwenyekiti
huyo alisema timu yao amepoteza baadhi ya wachezaji akiwemo Issa Rashid
“Baba Ubaya” aliyejiunga na wekundu wa Msimbazi Simba pamoja na Hussein
Javu anayesemekana kusaini yanga, lakini wana wachezaji wengine wa
kuziba nafasi zao na wengine watawasajili.
“Walikuwa
wachezaji muhimu sana, lakini hatuna jinsi, soka ni ajira yao, hatuna
uwezo wa kuwabania nafasi ya kucheza klabu nyingine, ila kiuhakika
tunao wachezaji wengi sana wa kuziba nafasi zao nab ado tunatafuta nyota
wengine wa kuwasainisha”. Alisema Baiser.
Akizungumzia
suala la Javu kusaini Yanga, Baiser alisema Mtibwa Sugar ilikuwa na
mkataba naye, lakini Yanga waliomba ruhusa ya kuzungumza naye na wao
wakakubali.
“Walituomba
kuongea na Javu, tuliwaruhusu. Kama wamekubaliana na kumpa mkataba sisi
bado hatuna taarifa ofisini, Yanga bado hawajaja kufanya taratibu za
uhamishoi, kwahiyo hatujui kama wameshamalizana naye, hivyo sitaki
kulizungumzia sana kwa sasa, wakati utafika nitazungumza”. Alisema
Baiser.
Baiser alisema Javu alikuwa mchezaji muhimu sana, lakini wanajipanga kutafuta mbadala wake.
0 comments:
Post a Comment