Mabingwa wa soka nchini Tanzania mwaka 1988, Wagosi wa kaya, wagosi wa ndima, Coastal Union, wenye makazi yao jijini Tanga, “waja leo waondoka leo” chini ya kocha Hemed Morroco wanaendelea vizuri na kambi yao ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara inayotarajiwa kuanza kushika kasi katika viwanja mbalimbali nchini Tanzania Agosti 24 mwaka huu.
Afisa habari wa klabu hiyo, Edo Kumwembe, amezungumza na MATUKIO DUNAINI na kusema kuwa wachezaji wote wamesharipoti kambini, na program ya mazoezi inakwenda vizuri.
“Wachezaji wote wapo salama, mwalimu anaendelea na program ya mazoezi huku akisisitiza kuwa malengo yake ni kutwaa ubingwa msimu ujao”. Alisema Kumwembe.
Kumwembe alisema kocha wao Hemed Morroco ameambiwa na viongozi wake kuwa wanahitaji kutwaa ubingwa, na yeye amekubaliana na mipango hiyo, hivyo kazi yake kubwa ni kunoa makali ya kikosi chake chenye wachezaji wakali ambao wamepewa motisha kubwa na viongozi.
Afisa habari huyo alisisitiza kuwa kutokana na usajili wao makini ambapo wamenasa baadhi ya mashine kama beki nguli kutoka kwa Wekundu wa Msimbazi Simba, Juma Said Nyoso, Kiungo fundi, mdogo wake Idd Moshi Mnyamwezi, namzungumzia Haruna Moshi Shaban “Boban” kutoka Simba, kiungo wa timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars ya Kenya, Chrispin Odula anayeungana na Mkenya mwenzake, kiungo wa zamani wa Simba, Fundi Jerry Santo, hakika watatwaa ndoo ya ligi kuu kama walivyofanya mwaka 1988.
“Msimu uliopita hatukufanya vibaya sana wala vizuri sana, haikuwa malengo yetu hata kidogo, sisi tulikuwa tunahitaji kuchukua ubingwa au kushika nafasi tatu za juu, kocha wetu Hemed Morroco alijitahidi sana, lakini mambo yalienda mrama, kwa msimu ujao tupo kamili gado”. Alisema Kumwembe.
Hivi karibuni viongozi wa Coastal Union chini ya Mkurugenzi wao wa Ufundi , Bin Slum walisema wanataka kuboresha mazingira mazuri kwa wachezaji wao kwa kuwapangia hoteli nzuri ili wafikirie soka tu na si vinginevyo na akiwezekana kujenga makazi yao ya kudumu ambapo wasaka kabumbu wao watakaa kwa raha zote na kula bata huku wakipigwa na viyoyozi kila kona.
0 comments:
Post a Comment