Hatimaye mtanange wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndaini (CHAN) kati ya Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya Uganda The Cranes katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam umemalizika kwa Stars kufungwa bao 1-0.
Bao la Uganda limefungwa dakika ya 46 na Gumma Dennis kufuatia makosa ya walinzi wa Stars walioongozwa na Agrey Moriss, Kelvin Yondan, Eresto Nyoni na Shomari Kapombe.
Stars walipata nafasi nyingi za kufunga, lakini safu ya ushambuliaji ilikuwa butu sana ikiongozwa na John Raphael Bocco “Adebayor” pamoja na Mrisho Ngassa .
Huduma ya Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu imeonekana kuhitajika katika mchezo wa leo kwani kuna nafasi ambazo nyota hao wa TP Mazembe ya DR Kongo huwa hawafanyi makosa.
Kikosi cha stars kilicheza vizuri, lakini kukosekana kwa umakini na ukabaji mbaya ndio sababu kubwa ya kufungwa na Waganda wanaonolewa na aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Rwanda “Amavubi”, mserbia Sredojvic Micho ambaye kwa sasa ndiye kocha mkuu wa Uganda huku akisaidiwa na Sam Timbe ambao kwa nyakati tofauti wameshawahi kuwa makocha wa mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara, Dar Young Africans.
Kufuatia matokeo ya leo, Taifa stars imejiweka katika mazingira magumu ya kufuzu fainali za CHAN kwani watahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili kusonga mbele.
Kama stars watashinda bao 1-0 ugenini, sheria itatumika kuamua njia gani itumike kumtafuta mshindi, inawezekana zitaongezwa dakika 30 na matokeo yakibaki hivyo hivyo, basi sheria ya penati itafuatia.
Lakini kama sheria ya kuongezwa kwa dakika haitatumika, basi mikwaju ya penati itaamua endapo tu Stars itakuwa inaongoza kwa bao 1-0 hadi dakika tisini zitakapokamilika.
Hata hivyo uzoefu unaonesha kuwa Uganda wanawapa shida sana Taifa stars na timu zote zinazotembelea uwanja wao wa taifa wa Nelson Mandele uliopo Namboole.
Kinachotakiwa kwa sasa ni kocha Kim Poulsen na wasaidizi wake kukaa chini na kutathimini makosa yaliyowagharimu katika mchezo wa leo ili kujipanga kuelekea mechi ya marudiano baada ya wiki mbili zijazo nchini Uganda.
Kim anatakiwa kuinoa safu yake ya ushambuliaji ambayo kwa siku ya leo imeshindwa kabais kfurukutu mbele ya mabeki wa Uganda ambao wameonekana kuwa makini na nguvu zaidi.
0 comments:
Post a Comment