Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi (waliokaa wapili kutoka kulia). picha kwa hisani ya Malafayaleleo.blogspot.com
Na Baraka Mpenja
WAKATI
Timu mbalimbali ligi kuu soka Tanzania bara zikianza maandalizi makali
ya msimu mpya wa ligi kuu unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 24
mwaka huu, nao wakali wapya wa ligi hiyo Mbeya City ya jijini Mbeya
wameanza kujifua chini ya kocha wao mkuu Juma Mwambusi.
Akizungumza na mtandao wa MATUKIO DUNIANI
kocha mkuu wa klabu hiyo Juma Mwambusi, amesema wachezaji kutoka
mikoani wameanza kuwasili kuanzia jana, huku akieleza kuwa anajipanga
kuongeza wachezaji wachache katika kikosi chake alichotoka nacho ligi
daraja la kwanza msimu uliopita.
“Wachezaji
wengi ni walewale, nina mpango wa kuongeza nyota wachache, wengi
nitawapandisha kutoka kikosi B, lakini wachezaji wengi waliopandisha
timu ligi kuu nimewaacha ila kuna nafasi chache nitaziba hivi karibuni”.
Alisema Mwambusi.
Mwambusi
alisema katika kikosi chake hana tabia ya kuwapa majina wachezaji kwa
kuwapa uhakika wa namba, kwani falsafa yake ni kuchezesha wachezaji wote
bila kujali majina yao.
“Mimi
siku zote falasafa yangu ni ileile, wachezaji wote wanaong`ara wameweza
kupata nafasi hiyo kwa sababu walipewa nafasi ya kucheza, hivyo
nitawapa wachezaji wote nafasi ya kucheza ili waongeze uzoefu”.
Alisisitiza Mwambusi.
Kuhusu
kusajili wachezaji wenye uzoefu mkubwa na mikikimikiki ya ligi kuu,
Mwambusi alisema hana mpango wa kusajili wakongwe kutokana na kikosi
chake kuwa na vijana wengi ambao wanafanya vizuri.
“Mbeya
City ina kikosi bora cha vijana, ninavyozungumza hapa kipo mkoani
Iringa wilaya ya Mufindi kushiriki michuano ya kombe la Muungano
Mufindi, ni kikosi kizuri sana, kinaongozwa na kocha wangu msaidizi Maka
Mwalwisyi ambaye anafanya kazi nzuri. Ni matumaini yangu hawa vijana ni
msingi mkubwa wa klabu yangu na watapewa nafasi”. Aliongeza Mwambusi.
Mwambusi
alisema kikosi chake kinahitaji kujifua kwa nguvu kuhimili mitanannge
ya ligi kuu, kwani ligi ya Tanzania bara imekuwa na ushindani mkubwa
sana.
“Ligi
imebadilika sana, niliifundisha Prisons miaka ya nyuma, sasa naona
mambo yamebadilika sana, lakini nina uhakika kwa uzoefu wangu
nitajipanga vizuri na kupambana hadi mwisho”. Alisema Mwambusi.
Mbeya
City ni miongoni mwa timu tatu zilizopanda ligi kuu soka Tanzania bara
msimu ujao, wakati nyingine ni Maafande wa Rhino Rangers ya Tabora, na
Ashanti United ya Dar es salaam.
Msimu
uliopita timu tatu za Africa Lyon ya Dar es salaam, Toto Africans ya
Mwanza na Polisi Morogoro zilishuka daraja na sasa zinaendelea na
mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi daraja la kwanza.
0 comments:
Post a Comment