Na Baraka Mpenja
KIUNGO
nyota wa klabu ya Simba, Wekundu wa Msimbazi “Taifa Kubwa” Ramadhan
Chombo “Redondo” wa Kitanzania mwenye mbwembwe na sifa kubwa ya kupaka
gozi rangi akiwa uwanjani, amesema hatima yake ya kuichezea klabu ya
hiyo msimu ujao itajulikana jumatatu ya wiki ijayo ambapo atakutana na
viongozi kuzungumzia suala lake.
Redondo amezungumza na MATUKIO DUNIANI na kuweka wazi kuwa bado ni mchezaji wa Simba kwani ana mkataba nao.
“Mimi
nina mkataba na Simba, mpaka sasa hatujazungumza lolote kuhusu hatima
yangu. Wiki ijao siku ya jumatatu kila kitu kitakuwa wazi ambapo
nitakutana na uongozi wa klabu yangu”. Alisema Redondo.
Kiungo
huyo mwenye uwezo wa aina yake aliongeza kuwa bado anahitaji kucheza
soka na kuitumikia klabu ya Simba licha ya kusimamishwa msimu uliopita
na aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Mfaransa Patrick Liewig kwa tuhuma za
utovu wa nidhamu.
“Tangu
msimu umeisha sijazungumza na viongozi wangu, bado nina nia ya
kuichezea klabu yangu. Mpira ni kazi yangu na naiheshimu sana”. Alisema
Redondo.
Redondo
hakusita kuweka wazi kuwa yuko tayari kusakata kandanda klabu yoyote ya
Tanzania endapo itafuatwa na kufanya mazungumzo yenye maslahi.
“Kama
sitapata nafasi ya kucheza Simba, naweza kujiunga na klabu yoyote ile
ya hapa nyumbani au nje ya nchi. Kikubwa ni maslahi kwani soka ndio kazi
yangu rasmi”. Alisema Redondo.
Nyota
huyo aliyeichezea Azam fc msimu wa 2011/2012 akitokea Simba na msimu wa
2012/2013 kurudi kwa wekundu wa Msimbazi Simba alisisitiza kuwa kwa
sasa anaendelea na mazoezi ya kujiweka sawa kwani anatambua kuwa soka
halina uchawi, bali ni mazoezi na kutambua wajibu wake.
“Kwasasa
naendelea na mazoezi binafsi, nasubiri hatima yangu Simba, nasisitiza,
nina mkataba na Simba, jumatatu nitasema nini hatima yangu”. Alisema
Redondo.
Chombo
ni miongoni mwa wachezaji waliokalia kuti la moto enzi za kocha
Mfaransa Patrick Liewig ambaye kwa sasa amefungashiwa virago na
kumuachia kocha mzawa Abdallah Kibadeni “King Mputa”.
Chombo
alituhumiwa na Liewig kuwa ni mtovu wa nidhamu, hivyo yeye na wenzake
akina Abdallah Juma, Ferlix Sunzu, Mwinyi Kazimoto, Paul Ngalema, Amir
Maftah, Haruna Moshi “Boban”, Juma Nyoso walisimamishwa na kocha Liewig.
Miongoni
mwa wachezaji hao, Mwinyi Kazimoto pekee ndiye aliyesajiliwa, huku
Ferlix Sunzu mkataba wake akimalizika, wakati wengine wametupiwa virago.
0 comments:
Post a Comment