Na Baraka Mpenja
Wakata miwa wa mashamba ya Manungu
Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar,
wanaendelea na hesabu zao za kuiwinda nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi kuu
soka Tanzania bara msimu huu.
Akizungumza na mtandao huu, msemaji
wa klabu hiyo, Tobias Kifaru Lugalambwike, amesema wanaendelea na mazoezi
makali ya kuwawinda vijana wa mitaa ya kishamapanda jijini Mwanza, Toto
Africans, mchezo utakaopigwa dimba la Manungu Complex aprili 10 mwaka huu.
“Hivi karibuni tumetoka kucheza na
ndugu zetu kule Kaitaba na kufungwa 3-1, sasa tumerejea katika mashamba yetu ya
Manungu tukiwasubiri Toto, tunajipanga vilivyo kuhakikisha tunajiweka mazingira
mazuri ya kupata angalau nafasi ya tatu au nne ya ligi kuu msimu huu”. Alisema Kifaru.
Kifaru alisema msimu huu kila
mchezaji ametambua kuwa soka ni ajira yake na ndio maana ligi imekuwa na
changamoto kubwa huku kila timu ikihitaji kupata mafanikio mazuri.
Msemaji huyo aliongeza kuwa wao wamesaliwa
na michezo minne ambayo watakutana na daluga za Africa Lyon, Toto Africans, JKT
Oljoro, na JKT Ruvu, hivyo wanaijenga timu kuhakikisha wanashinda mitanange
yote iliyobakia.
“Mwalimu Merck Mexeme anawafua vizuri
sana wachezaji wetu, yeye anaelewa matatizo ya timu, kwa hiyo imani yetu ni
kuibuka na ushindi dhidi ya vibonde hao wa ligi kuu Toto africans walioko nafsi
ya mkiani”. Alijigamba Kifaru.
Akizungumzia hali ya mchezo wenyewe,
Kifaru alisema Toto wanapigana kufa na kupona kukwepa mkasi wa kushuka daraja,
wao wanahitaji nafasi nzuri katika msimamo, hivyo sura ya mchezo huo inaonekana
kuwa ngumu licha ya maandalizi makubwa wanayofanya kwa sasa.
Pia alisisitiza kuwa wao wapo nafasi
ya sita katika msimamo, lakini waliopo juu yao yaani Azam fc, Simba, kagera
sugar, Coastal union wakikosea hesabu zao basi Mtibwa itapata nafasi nzuri
mwishoni mwa msimu.
Kifaru aliwata mashabiki wa klabu
hiyo kuondosha mashaka kwani wamejipanga barabara hivyo ni muhimu kwao kufika
kwa wingi Manungu Complex wiki ijayo kuishangilia timu hiyo bora nchini
Tanzania.
Mbali na mchezo huo wa jumatano ijayo,
nao vinara Yanga watavaana na JKT Oljoro uwanja wa taifa, Tanzania Prisons
watakuwa nyumbani kwao Sokonne kumenyana na Mgambo JKT, Polisi Moro watakuwa
Jamhuri kuvaana na Ruvu Shooting, wagosi wa kaya Coastal unioni watakuwa kwao
Mkwakwani kupepetana na JKT Ruvu, na Azam fc baada ya leo kucheza kombe la
shirikisho na Barrack Yc ya Liberia watawakaribisha Africa Lyon dimba la
chamazi.
0 comments:
Post a Comment