
Na Baraka Mpenja
Kufuatia mchezo wa
riadha kushuka nchini, Chama cha riadha mkoani Pwani kwa kushirikiana na chama
cha riadha Tanzania (RT) kinaendesha mafunzo maalumu ya kufundisha kozi za ukocha wa mchezo
huo zinazoendelea mjini Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza na mtandao
huu kutoka Kibaha, mmoja wa wakufunzi wa
mafunzo hayo , katibu mkuu wa RT Suleiman Nyambui amesema mafunzo hayo yana
lengo la kupata wataalamu mbalimbali nchini Tanzania.
“Riadha ni miongoni
mwa michezo mashuhuri duniani, ukirudi miaka ya sabini, Tanzania ilikuwa
inaogopeka kimataifa katika mchezo huu, nadhani unawakumbuka akina Bayi na
Nyambui, sasa tunataka kurudisha hadhi ya mchezo huu unaozidi kushuka”. Alisema
Nyambui.
Katibu huyo wa RT
alisema kuwa mafunzo hayo yanayoendelea kibaha yamejumuisha waalimu kutoka
mikoa ya Songea, Geita, Mara, Morogoro, Rukwa huku waalimu wengi wawakitokea
mkoa wa Pwani.
Nyambua aliongeza
kuwa leo walikuwepo madaktari wa viungo kutoka wizara ya Vijana, utamaduni na michezo
ambao wamefundisha namna ya kugundua na kuwatibu wanariadha wapatapo majeruhi.
Mafunzo hayo
yatamalizika jumamosi ya wiki hii kwa wahitimu hao kutunukiwa vyeti katika
hafla maalumu itakayoandaliwa mjini Kibaha.
Akizungumzia mkakati
wa RT, Nyambui alisema kuwa ifikapo mwaka 2020 watahakikisha kila shule Tanzania
ina mwalimu mtaalamu wa kufundisha riadha kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Nyambui alisisitiza
kuwa suala hilo litafanikiwa kwa kushirikiana na viongozi wa serikali, wadau wa
michezo na watanzania wote kwa ujumla.
“Tukikubali umuhimu
wa mchezo huu kwa taifa,tutaweza kufika mbali na kuwafikia wenzetu wa Ethiopia,
Kenya na wengine ambao wanafanya vizuri zaidi katika mchezo huo”. Alisema Nyambui.
Katibu huyo alisema
wakati huu si mwafaka kuandaa timu kwa ajili ya Olmpiki wala michuano yoyote ya
kimataifa, bali ni wakati wa kufumbia macho michuano hiyo ili nafasi ya kujenga
misingi ya mchezo huo ipatikane.
Nyambui aliongeza
kuwa kwa sasa wanajipanga kuzunguka mikoa yote ili waongea na maafisa michezo, pamoja
na maafisa elimu ili kila shule iwe inafundisha riadha.
0 comments:
Post a Comment