Na Baraka Mpenja
Siku moja baada ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kumtaka mshambuliaji ,Nsa Job Mahinya ,wa
Coastal Union kuwasilisha maelezo yake juu ya madai kuwa alipewa rushwa ya sh.
milioni mbili ili asiifunge moja ya timu vigogo vya soka nchini, katibu mkuu wa zamani wa shirikisho hilo,
Fredrick Mwakalabela, amesema suala hilo limechukuliwa kwa uharaka sana.
Mwakalabela amesema kauli
ya kumwambia kuwa, TFF itachukua hatua kali dhidi ya yake iwapo hatawasilisha
maelezo yake kuhusiana na suala hilo ingelenga kumtumia nyota huyo kama chanzo cha
taarifa zaidi zinazohusu masuala ya
Rushwa michezoni kwani tatizo hilo lipo hususani mwishoni mwa ligi.
“Kuna mambo mengi
yalijitokeza miaka ya nyuma, unakumbuaka suala la Ulimboka Mwakingwe na akina
Shabaan Kado wakati simba ilikwenda Morogoro, sidhani kama lilichukuliwa hatua
sutahiki,na ndio maana mambo haya yanaendelea kujitokeza chini kwa chini”.
Alisema Mwakalabela.
![]() |
NSA JOB MAHINYA |
Mwakalebela alisema
kuwa , kuna watu wachache wanaotia doa soka letu kutokana na mazoea ya kucheza
mchezo mchafu na kupanga matokeo katika mechi muhimu.
Katibu huyo mkuu wa
zamani wa TFF alisema kuna wakati Fulani wachezaji hucheza chini ya kiwango wakidaiwa
kuwa na mapenzi na timu Fulani wakitarajia kusajiliwa, lakini mambo haya
hupuuzwa.
Mwakalebela aliongeza
kuwa ,wachezaji wanafahamiana nani kachukua rushwa katika mchezo fulani, cha
msingi ni kusimama kidete kupiga vita mchezo huu mchafu unaomaliza kiwango cha
soka letu.
Katibu huyo wa zamani
wa TFF alisema pia waamzi mara kwa mara wanatuhumiwa kupokea hongo ili
kuzisaidia timu fulani.
“Sauala la waamuzi
pia linatakiwa lichukuliwe kwa uzito wa juu, kuna mambo fulani yanajitokeza katika
michezo, hakika yanatia hofu kubwa, ukifuatilia ripoti za waamuzi huwa
zinafanana sana, lakini ukishihudia mchezo unaweza kugundua kuwa kuna uhuni umefanyika”.
Aliongeza Mwakalebela.
Mwakalabela
alisisitiza kuwa wakati akiwa kiongozi waamuzi na makamisaa wa mechi walikuwa
wanaandika ripoti inayofanana hata kama kulikuwa na matatizo, suluhisho ni kuwepo mwangalizi maalumu wa
waamuzi na hali ya mchezo husika ili kama kuna mambo yasiyoeleweka wahusika wachukuliwe
hatua zinazostahiki.
Katibu mkuu huyo wa
zamani wa TFF alishauri kuwa mambo haya yaangaliwe kwa jicho la tatu, na kama
yatapuuzwa timu zinazojihusishwa na uozo huu zitaendelea kuumbuka kimataifa,
pia timu ya taifa itakosa wachezaji wazuri.
Taarifa kutoka TFF
hapo jana zilieleza kuwa Job alikaririwa Aprili 3 mwaka huu na kituo cha redio
cha Clouds FM katika kipindi cha Amplifier kuwa alipewa kiasi hicho cha fedha
na kiongozi wa timu husika ili asiifunge katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom,
lakini alipokea fedha hizo na kuifunga timu hiyo.
Baadaye kiongozi huyo
alikuwa akimtaka arejeshe fedha hizo. Pia TFF imekiandikia kituo hicho cha
redio kutaka nakala ya kipindi hicho ili pamoja na maelezo ya mshambuliaji huyo
vipelekwe katika Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
0 comments:
Post a Comment