Ligi kuu soka Tanzania bara msimu
wa 2012/2013 imeendelea kushika kasi leo hii kwa michezo miwili kupigwa
katika miji ya Mbeya na Dar es salaam.
Katika dimba la kisasa la Taifa
maeneo ya Chang`ombe jijini Dar es salaam, mabingwa wa kombe la kagame
na vinara wa ligi hiyo Klabu ya Yanga imeendelea kujikita zaidi kileleni
baada ya leo hii kushusha kipondo cha mabao 3-0 kwa maafande wa JKT
Oljoro kutoka jijini Arusha“Geneva ya Afrika”.
Mabao ya Yanga yamefungwa na
wachezaji Nadir Haroub `Canavaro`, winga machachari na mwenye kasi ya
ajabu Simon Msuva pamoja na mtaalamu kutoka Uganda Khamis Kiiza `Diego
wa Afrika Mashariki`.
Kwa matokeo hayo Dar Young
Africans wamefikisha pointi 52 kileleni na kuwaacha Azam fc pointi 6
nyuma ambao kesho wanaingia kibaruani kumenyana na mnyama pori, wekundu
wa Msimbazi Simba `Taifa Kubwa` katika dimba maridhawa la Taifa jijini
Dar es salaam.
Wakati Yanga waking`ara mjini,
jijini Mbeya Uwanja wa kumbukumbu ya Hayati Edward Moringe Sokoine
umeendelea kutia baraka kwa maafande wa jeshi la magereza Tanzania
Prisons “wajelajela” baada ya leo hii kupata ushindi muhimu wa mabao 2-0
dhidi ya vijana watukutu wa Charles Boniface Mkwasa “Master”, klabu ya
Ruvu Shooting kutoka mkoani Pwani.
Mabao ya Prisons yametiwa kambani kipindi cha pili na mshambuliaji mwenye manjonjo mengi Elias Maguli katika dakika ya 56 na 60.
Akizungumza na mtandao huu katibu
mkuu wa Prisons Sadick Jumbe alisema mchezo huo ulikuwa mgumu sana kwao
kutokana na ubora wa wapinzani wao.
“Shooting walicheza vizuri sana,
lakini tulijiandaa kutafuta ushindi huku tukiwa na kumbukumbu nzuri ya
kuwafunga Mgambo JKT bao 1-0 jumatani ya wiki hii, hivyo tulichagizwa na
matokeo yale na ndio maana leo hii tumecheza kwa uangalifu mkubwa”.
Alisema Jumbe.
Jumbe aliongeza kuwa mashabiki wa soka mkoani humo wameendelea kujitokeza kwa wingi na kuwapa hamasa wachezaji wao.
Akiwazungumzia Shooting, Jumbe
alisema maafande hao walicheza vizuri na kumaliza dakika 45 za kipindi
cha kwanza bila kufungwa, lakini kipindi cha pili kocha wa Prisons
Jumanne Chale aliwatuliza vijana wake na kuanza kuwakimbiza mchakamchaka
wa jeshi wapinzani wao na hatimaye kupachika mabao mawili kambani.
Kwa upande wao Ruvu shooting
kupitia kwa afisa habari wake Masau Bwire walisema waamuzi wa mchezo huo
hawakuchezesha kihalali kwani kuna makosa mengi yaliyojitokeza.
“Sasa kuna mambo yanatokeo sisi
hatuelewi, vijana wetu huwa wana nidhamu sana lakini leo hii
walichachamaa kutokana na maamuzi ya utata, sisi tunadhani kamati ya
saidie Prisons ishinde itakuwa imeshafanya mambo yake, hakika kwa madudu
haya hakuna mpira Tanzania”. Aliongea Masau kwa masikitiko.
Afisa habari huyo ameongeza kuwa
endapo TFF kupitia kamati ya ligi hawataangalia kamati hizi, mwisho wa
soka letu utafikia muda mfupi ujao.
0 comments:
Post a Comment