
Na Baraka Mpenja
Shirikisho la soka Tanzania TFF
limeshauriwa kuchunguza kwa makini kamati zinazoundwa kienyeji kusaidia baadhi
ya timu za ligi kuu kushinda michezo yake ya nyumbani wakati huu wa dakika za
lala salama.
Maafande wa Ruvu Shooting kupitia kwa
afisa habari wake, Masau Bwire, wamesema kutokana na aina ya wajumbe wanaounda
baadhi ya kamati hizo kuwa viongozi wenye dhamana ya kuongoza soka mikoani, kamati
hizo haziaminiki tena.
Masau alisema suala la viongozi wa
vyama kuwa wajumbe wa kamati hizo linaleta wasiwasi wa kupanga matokeo kwa
kuwasaidia wenyeji.
“Ikumbukwe kuwa viongozi ndio
wanaowapokea waamuzi na timu pinzani, sasa viongozi hawa wanapoongoza kamati
hizo, hakika kunakuwepo na dalili za kufanya hujuma kwa wageni”. Alieleza Masau
Afisa habari huyo aliongeza kuwa
hatua hii ya lala salama ambayo baadhi ya timu zinahangaika kushuka daraja,
kuna baadhi ya waamuzi wanaboronga sana na kuleta wasiwasi.
Masau aliwata TFF kuangalia kwa jicho
la tatu kamati hizi ili kama kuna mazingira ya rushwa wahusika wachukuliwe
hatua kali za kisheria.
“Unajua kuna mazingira yanaweza
kutengenezwa katika mchezo fulani halafu yakakulazimisha kuamini kwamba kuna madudu
yanafanyika, hali ya kamati hizi ni hatari sana, endapo TFF wataona ni suala la
kawaida, hakika litaleta madhara makubwa”. Alionya Masau.
Hivi karibuni mkoa wa Morogoro
viongozi wa timu ya polisi Morogoro walikariri wakisema kumeanzishwa kamati na
kampeni maalumu ya kuisaidi timu ya Polisi Moro isishuke daraja.
Pia jijini Mbeya kumetokea hali kama
hiyo, viongozi wa chama cha soka wameunda kamati ya kuisaidia Prisons isishuke daraja
msimu huu. Kamati hiyo ipo chini ya kamanda wa polisi wa mkoa huo, Diwani
Athman Msuya akishirikiana na wadau wa soka.
Kufuatia hali hiyo kuendelea kutanda
wingu la ligi kuu ligi kuu, Ruvu shooting walishauri suala hilo kuangaliwa kwa
undani kwani kuna dalili ya kuhujumu timu pinzania mchezoni.
0 comments:
Post a Comment