Na Boniface Wambura
KAMATI YA UTENDAJI TFF KUJADILI TAMKO LA SERIKALI
Sekretarieti
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepokea barua ya
Serikali ikielezea uamuzi wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Dk. Fenella Mukangara kutengua uamuzi wa Msajili wa Klabu na
Vyama vya Michezo nchini kuidhinisha marekebisho ya Katiba ya TFF toleo
la 2012.

Baada
ya kupokea barua hiyo jana alasiri (Februari 25 mwaka huu),
Sekretarieti iliwasiliana na Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye ameagiza
kuitishwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji kujadili tamko hilo.
Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji ya TFF kitafanyika Jumamosi (Machi 2 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
KOCHA AZAM AFUNGIWA KWA KUCHOJOA BUKTA
Kocha
Mkuu wa Azam, Stewart John Hall amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini
ya sh. 500,000 kwa kushusha bukta yake na kumlalamikia mwamuzi msaidizi
wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu yake na Kagera
Sugar iliyochezwa Januari 26 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ulioko
Chamazi, Dar es Salaam.
Adhabu
hiyo imetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) iliyokutana mwishoni mwa wiki kupitia ripoti za michuano
ya VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2012/2013 inayoendelea
hivi sasa na kufanya uamuzi mbalimbali.
Naye
Kocha Msaidizi wa timu ya Mgambo Shooting, Denis Mwingira ametozwa
faini ya sh. 500,000 kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi kwenye mechi dhidi
ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Oktoba mwaka jana katika Uwanja wa Manungu.
Ally
Jangalu ambaye ni Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro naye ameangukiwa na
rungu la Kamati ya Ligi kwa kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya
kutolewa kwenye benchi kwa kupinga uamuzi wa refa kwa sauti ya juu.
Alitenda kosa hilo kwenye mechi kati yao na Kagera Sugar iliyochezwa
Novemba 10 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Matukio
ya aina hiyo kwa kocha Jangalu yamekuwa ya kujirudiarudia ambapo Oktoba
13 mwaka jana katika mechi dhidi ya Azam iliyochezwa mjini Morogoro
aliondolewa na mwamuzi kwenye benchi kwa kuchochea wachezaji wa timu
yake wacheze rafu.
Naye
Kocha wa timu ya Moro United inayoshiriki FDL, Yusuf Macho amepigwa
faini ya sh. 200,000 kwa kumtolea lugha chafu refa baada ya mechi dhidi
ya Transit Camp iliyofanyika Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Mabatini
mjini Mlandizi.
Pia
Kocha wa Burkina Faso, Hasheem Mkingie amepigwa faini ya sh. 200,000
baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kutoa lugha chafu katika mechi ya
FDL dhidi ya Mkamba Rangers.
Kiongozi
wa Majimaji, Joseph Nswila ambaye aliingia uwanjani baada ya mechi
dhidi ya Mlale JKT kumalizika na kuvamia waamuzi amefungiwa miezi sita.
Vilevile
timu ya Azam imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika
uwanjani kwenye mechi kati yao na JKT Oljoro iliyochezwa Novemba 7 mwaka
jana katika Uwanja wao wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Pia
Coastal Union imetozwa faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki wake
kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili wakati wa mechi yao
dhidi ya Simba iliyochezwa Oktoba mwaka jana Uwanja wa Mkwakwani jijini
Tanga.
Nayo
klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa timu yake
kugoma kuingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo wakati wa mapumziko
katika mechi dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga, Oktoba 24 mwaka jana.
Timu
ya Burkina Faso ya Morogoro imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na
kuonesha vitendo vya ushirikina kabla ya mechi yao dhidi ya Mbeya City
iliyochezwa Oktoba 24 mwaka jana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Faini
ya ushirikina ya sh. 200,000 pia imepigwa timu ya Pamba baada ya
kuonesha vitendo hivyo kwenye mechi yao dhidi ya Mwadui iliyochezwa
Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Nayo
Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya washabiki wake
kumtolea lugha chafu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro
(MRFA), Hamis Semka na kumrushia chupa za maji mwamuzi wa mezani katika
mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa mjini Morogoro.
Polisi
Dodoma imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuvamia
uwanjani na kutaka kuwapiga waamuzi katika mechi yao dhidi ya JKT
Kanembwa na kusababisha mipira miwili ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Dodoma (DOREFA) kupotea.
Pia
klabu kadhaa zimeandikiwa barua za onyo kwa timu zao kuchelewa kufika
uwanjani au kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match
meeting). Klabu hizo ni Coastal Union, JKT Ruvu, Toto Africans, Simba,
Green Warriors, Majimaji, Mkamba Rangers, Polisi Dodoma, JKT Kanembwa,
Moro United.
Mchezaji
Stanley Nkomola wa JKT Ruvu baada ya mechi dhidi ya Coastal Union
alikwenda jukwaani na kuanza kupigana na washabiki. Pia kipa wa timu ya
Transit Camp, Baltazar Makene baada ya mechi dhidi ya Tessema aliruka
uzio na kwenda kupigana na washabiki.
Kwa
vile masuala ya wachezaji hao ni ya kinidhamu yamepelekwa kwenye Kamati
ya Nidhamu inayoongozwa na Kamishna wa Polisi (CP) mstaafu Alfred
Tibaigana kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
MWAMUZI FIFA, MAHAGI WAONDOLEWA VPL
Mwamuzi
Msaidizi wa FIFA, Ferdinand Chacha ameondolewa kuchezesha mechi za VPL
baada ya kupata alama za chini kwenye mechi kati ya African Lyon na
Simba iliyochezwa mwezi uliopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Waamuzi
wanaopata alama 6.5 au chini ya hapo kati ya 10 zinazohitajika pia
wanaondolewa kwenye mechi za VPL na FDL.
Waamuzi
wengine walioondolewa kwa kutomudu mechi walizochezesha za VPL ni
Mathew Akrama (Yanga vs Simba), Ephrony Ndissa (Yanga vs Simba), Ronald
Swai (Yanga vs Mtibwa Sugar).
Walioondolewa
kwa kupata alama za chini ni Alex Mahagi (Simba vs JKT Ruvu), Methusela
Musebula (Toto Africans vs Coastal Union), Lingstone Lwiza (Toto
Africans vs Coastal Union), Idd Mikongoti (Toto Africans vs Mtibwa
Sugar) na Samson Kobe (Toto Africans vs Mtibwa Sugar).
Masoud
Mkelemi aliyekuwa mwamuzi wa mezani katika mechi ya FDL kati ya Moro
United na Villa Squad ameondolewa kwa kutofika kwenye mkutano wa
maandalizi ya mechi (Pre-match meeting) na alichelewa kwa dakika tano
kufika uwanjani.
MAKAMISHNA VPL/FDL WASIMAMISHWA, WAONYWA
Baadhi
ya makamishna wa VPL na FDL wameondolewa na wengine kusimamishwa
kusimamia mechi za ligi hizo kutokana na upungufu kwenye ripoti zao au
kutowasilisha kabisa ripoti hizo TFF baada ya mechi.
Kamishna
Mohamed Jumbe aliyesimamia mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba
ameondolewa kwenye orodha ya makamishna kutokana na ripoti yake kuwa na
upungufu.
Makamishna
wa mechi kati ya JKT Oljoro vs Yanga (Hakim Byemba), JKT Oljoro vs
Kagera Sugar (Salum Kikwamba), Toto Africans vs African Lyon (Charles
Komba), Coastal Union vs JKT Oljoro (Mohamed Nyange) wamesimamishwa hadi
watakapowasilisha ripoti zao TFF.
Kwa
upande wa FDL makamishna waliosimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti
zao TFF ni wa mechi kati ya Kurugenzi vs Polisi Iringa, Morani vs
Mwadui, Polisi Mara vs Pamba, Polisi Mara vs Mwadui, Morani vs JKT
Kanembwa na Pamba vs Polisi Dodoma.
Wengine
ni Mwadui vs JKT Kanembwa, Polisi Tabora vs Morani, Polisi Dodoma vs
Polisi Mara, Polisi Tabora vs Mwadui, Polisi Mara vs Morani, JKT
Kanembwa vs Polisi Mara, Morani vs Rhino Rangers na Small Kids vs Mkamba
Rangers.
Kamati
ya Ligi imewakumbusha makamishna wote kuwa ni jukumu lao kuhakikisha
ripoti zao zimefika TFF na kurekebisha upungufu wa jinsi ya kuripoti
matukio yanayotokea uwanjani. Licha ya kutuma nakala kwa njia ya email,
wanatakiwa pia kuwasilisha ripoti halisi (original) TFF.
MECHI YA SIMBA, MTIBWA YAINGIZA MIL 62/-
Mechi
namba 121 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa juzi (Februari 24 mwaka
huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Mtibwa
Sugar kuibuka ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba imeingiza sh.
239,686,000.
Watazamaji
10,669 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa
sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata
mgawo wa sh. 14,577,252.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
iliyolipwa ni sh. 9,467,694.92.
Kiingilio
cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata
tiketi hizo walikuwa 9,491 na kuingiza sh. 47,455,000 wakati idadi ndogo
ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki
105 na kuingiza sh. 2,100,000.
Mgawo
mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,412,162.26,
tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 4,447,297.36, Kamati ya Ligi
sh. 4,447,297.36, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
2,223,648.68 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA)
sh. 1,729,504.53.
VUMBI LA VPL KUENDELEA JUMATANO
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Februari 27 mwaka huu) kwa mechi tano zitakazochezwa katika viwanja tofauti.
Vinara
wa ligi hiyo Yanga wataikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam kwa viingilio vya sh. 5,000 (viti vya bluu na kijani), sh.
8,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 15,000 (VIP C na B) na sh.
20,000 (VIP A).
Mechi
nyingine za ligi hiyo ni Coastal Union vs Ruvu Shooting (Mkwakwani,
Tanga), Polisi Morogoro vs Mgambo Shooting (Jamhuri, Morogoro), JKT Ruvu
vs Toto Africans (Azam Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar vs
Tanzania Prisons (Manungu, Morogoro).
0 comments:
Post a Comment