
Kocha wa klabu ya Manchester City, Pep Guardiola ameweka wazi kuwa hatoweza kumchagua mchezaji Yaya Toure katika kikosi chake chochote mpaka pale atakapoweza kuomba msamaha kwa klabu na wachezaji wenzie kutokana na maneno ya shutuma aliyoyatoa wakala wake.
Toure, 33, amefanikiwa kucheza mchezo mmoja tu mpaka sasa tangu msimu huu uanze huku pia mapema msimu huu akienguliwa katika kikosi cha Manchester City ambacho kinashiriki klabu bingwa barani Ulaya.
Wakala wa Yaya Toure, Dimitri Seluk, alisema kuwa mteja wake kadhalilishwa na kuwa kocha wake Pep Guardiola anatakiwa aombe radhi kwa klabu hiyo iwapo klabu hiyo haitoshinda michuano hiyo inayoendelea.
Guardiola alisema: “anatakiwa kuomba radhi, na kama ataamua kutokufanya hivyo basi hatocheza katika kikosi changu”. Pep Guardiola pia ametaka wakala huyo, Seluk, aombe radhi.
Pep aliongeza pia ilikuwa ngumu sana kwake kuweza kumuacha Toure nje ya kikosi cha Ulaya.
“Kama ana tatizo kuna watu ndani ya klabu anaoweza kuzungumza nao na kutatua mambo yake,” alisema Guardiola ambaye pia alihusika kumuondoa Toure katika klabu ya Barcelona mwaka 2010.
Guardiola alisema yote haya muda mfupi baada ya Yaya Toure kutangaza kuachana na soka la timu ya Taifa.
Yaya alianza kucheza timu ya Taifa ya the Ivory Coast mwaka 2004, akiichezea timu hiyo michezo 113 ya ushindani, na akifanikiwa kushinda taji la mataifa ya Afrika mwaka 2015.
0 comments:
Post a Comment