
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga wameamua kwenda kujichimbia kisiwani Pemba na kuzima mianya ya Al Ahly ya Misri kuona mbinu zao ambao watakutana Aprili 9 mwaka huu katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Taarifa ambazo BINGWA limezipata kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, zinasema kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van de Pluijm, amependekeza kikosi chake kiende kuweka kambi Pemba kutokana na utulivu uliopo huko.
Chanzo hicho kilisema timu yao ikiwa kisiwani humo itaweza kujiandaa vizuri kutokana na utulivu mkubwa uliokuwepo, lakini wapinzani wao hawataweza kuona maandalizi yao ya mwisho.
“Pemba kuna utulivu wa asilimia 100, unapojiandaa na mechi kubwa kama ya Al Ahly wachezaji wanahitaji sehemu tulivu ya kujiandaa ambayo ni ngumu kukutana na bugudha yoyote.
Tunapopiga kambi Pemba hakuna mchezaji anayetoka nje ya kambi, kila mmoja anakuwa ndani na ni salama kwao kimpira, baada ya benchi la ufundi kupendekeza hilo tuliona sawa kwani tupo kwa ajili ya kutimiza mahitaji yake ambayo yatatuhakikishia tunapata matokeo bora,” alisema mtoa habari huyo.
Yanga wamekuwa na mafanikio wanapotokea Pemba kujiandaa na michezo mbalimbali ikiwemo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwani wamekuwa wakirejea Dar es Salaam na kupata matokeo mazuri.
Mara mbili timu hiyo ilipoweka kambi Pemba, iliibuka na ushindi dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba katika mechi za Ligi Kuu msimu huu, hivyo jambo hilo huenda limewavutia tena kwenda kujiandaa na mechi yao dhidi ya Wamisri hao ambao ni timu ngumu.
Mara ya mwisho Yanga na Al Ahly zilipokutana kwenye Uwanja wa Taifa, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, lakini ilitolewa kwa mikwaju ya penalti baada ya kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano uliofanyika jijini Alexandria nchini Misri.
Mabingwa hao watetezi Bara, walifanikiwa kuvuka hatua ya 16 bora baada ya kuitoa APR ya Rwanda kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2.
Credit:Bingwa
0 comments:
Post a Comment