
YANGA washindwe wenyewe kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya siri zote kuhusiana na ubora na udhaifu wa wapinzani wao wa raundi ya 16, Al Ahly kuwa hadharani ikiwamo dakika ambazo iwapo kocha wa Wanajangwani hao, Hans van der Pluijm atazichanga vema karata zake, Mholanzi mwenzake Martin Jol atakiona cha moto.
Yanga na Al Ahly zinatarajiwa kukutana katika mchezo wa kwanza Aprili 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye ambapo mshindi wa jumla atatinga hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Pamoja na ubora wa kikosi cha Al Ahly chenye wachezaji walionunuliwa kwa dau hadi Sh bilioni nne, tofauti na Yanga ambako aliyezoa fedha nyingi zaidi ni Sh milioni 100, bado wameonekana kucheza kwa mtindo wa ‘homa ya vipindi’.
Utafiti uliofanywa na BINGWA umebaini kuwa tangu msimu wa 2010 hadi sasa, Al Ahly wamekuwa wakifunga mabao yao kati ya dakika ya kwanza hadi ya 30 na baada ya hapo, hupunguza kasi yao ya mashambulizi kabla ya kuibuka tena kuanzia kati ya dakika ya 60 hadi 90.
Kwa maana hiyo, iwapo timu pinzani itamudu kuzichanga karata zake vema na kuibana timu hiyo kutopata mabao ndani ya dakika hizo, ijue imelamba dume mbele ya vinara hao wa soka Afrika wenye maskani yao jijini Cairo ikiwa imeanzishwa Aprili 24, mwaka 1907.
Hali kadhalika, timu inayocheza na Al Ahly ambayo mwaka 2000 ilitajwa rasmi na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kama Klabu Bora ya Karne ya Afrika, inatakiwa kuhakikisha inajipanga kufanya mashambulizi ya nguvu kuanzia dakika ya 35 hadi 45 za kipindi cha kwanza, muda ambao ni mwafaka kuwafunga kirahisi Waarabu hao wakati wakiwa wanakosa nguvu baada ya kuhaha kusaka mabao bila mafanikio ndani ya dakika 30 za mwanzo.
Lakini iwapo wapinzani wa timu hiyo wakiwamo Yanga kuelekea mechi yao na vigogo hao, watashindwa kupata mabao ndani ya dakika 20 za mwisho za kipindi cha kwanza, inatakiwa kuanza kipindi cha pili kwa kasi ya hali ya juu na kufanya mashambulizi ya nguvu ili kupata mabao kabla ya wapinzani wao hao kucharuka dakika 30 za mwisho kama ilivyo kawaida yao.
Mathalani, katika mchezo wao wa Ligi Kuu Misri Februari 18 mwaka huu dhidi ya Ghazl Al Mahalla, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, bao la Al Ahly likipatikana dakika ya 90+5 kupitia kwa Ramadan Sobhi, ikiwa ni baada ya Mhammed Yahia kuanza kuifungia timu yake dakika ya 48.
Februari 23, mwaka huu dhidi ya Al Masry ulioishia kwa sare ya mabao 2-2, mabao yao yalipatikana dakika ya 26 kupitia kwa Momen Zakaria na dakika ya 78 mfungaji akiwa na Malick Evouna, wakati yale ya wapinzani wao yaliwekwa kimiani na Ahmed Yasser dakika ya 11 na Mohamed Magdy dakika ya 58.
Machi 2, mwaka huu waliichapa Petrojet mabao 2-0, yakipatikana dakika za 62 na 67, yote yakiwekwa kimiani na El Said Abdallah, wakati siku tatu baadaye waliifunga Misri Lel Makasa mabao 2-1 yaliyopatikana dakika za 42 na 72 kupitia kwa Sobhi na Amri Gamal, huku lile la wapinzani wao likifungwa dakika ya 59 na Mohammed Gaber.
Machi 12 walivaana na Recreativo do Libolo ya Angola katika mchezo wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutoka suluhu, kabla ya wababe hao kushinda mabao 2-0 timu hizo ziliporudiana nchini Misri ambapo mabao yao yalifungwa dakika ya 10 na 83 na Sobhi na John Antwi.
Kutokana na hali hiyo, ni wazi iwapo Yanga watafanikiwa kuwabana Al Ahly dakika 30 za kwanza na kuishambulia kwa nguvu timu hiyo kuanzia dakika ya 30, watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kushinda, lakini tu iwapo kila mchezaji atacheza kwa nidhamu ya hali ya juu kuepuka kufanya kosa lolote ambalo linaweza kuwa faida kwa wapinzani wao hao au kumponza na kuonyeshwa kadi.
Na sasa wakati uongozi wa Yanga chini ya mwenyekiti wake, Yusuf Manji na benchi zima la ufundi wakiwa na ‘faili’ zima la ubora na udhaifu wa Al Ahly, ni wazi kazi iliyobaki kwao ni rahisi mno, kuhakikisha wanafanyia kazi kila kitu ambacho kinaweza kuwa mtaji kwao wa kuwatoa Waarabu hao.
Ikumbukwe kuwa uongozi wa Al Ahly kwa sasa unahaha jinsi ya kuisoma Yanga, kitendo ambacho kinaweza kuwa somo kwa Manji na timu yake, kuona ni vipi wanaijengea timu yao mazingira ya ushindi mnono katika mchezo wa kwanza, ili kujijengea mazingira mazuri ya kusonga mbele kuelekea mchezo wa marudiano ugenini.
Juu ya hilo, Manji alipoulizwa na BINGWA mikakati yao kuelekea mechi dhidi ya Al Ahly, hakutaka kuweka wazi hilo akimtupia mpira kocha Pluijm akidai kuwa mipango yote ipo mikononi mwa Mholanzi huyo.
“Siwezi kuzungumzia lolote juu ya mikakati yetu, unaweza kuwasiliana na kocha mkuu, yenye ndiye anayefahamu kila kitu,” alisema Manji.
Kwa upande wake, Pluijm ameweka wazi kikosi chake kutokuwa na mchecheto wa kuwavaa wapinzani wao hao, akiahidi kufanya vizuri.
“Tuna kikosi kizuri kinachoweza kuifunga timu yoyote, iwe ni katika ligi ya ndani ya michuano ya kimataifa, hivyo mashabiki wa Yanga waendelee kutuunga mkono kama ambavyo wamekuwa wakifanya,” alisema.
0 comments:
Post a Comment