Issofou Aboubacar Garba
HAKUNA mafanikio bila mipango. Kocha wa Yanga Hans Pluijm anawaangalia kwa jicho refu wachezaji wawili tegemeo wa APR ya Rwanda ambao kuna uwezekano mkubwa akatangaza lolote miezi michache ijayo, hasa Yanga ikitinga kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pluijm amewataja kiungo mkabaji wa APR, Yannick Mukunzi pamoja na winga wa kushoto Patrick Sibomana. Lakini habari za ndani zinadai kwamba anamlia mingo zaidi Sibomana ambaye amepata picha kwamba anaweza kuvaa jezi ya winga Issofou Aboubacar ‘Diego’ raia wa Niger ambaye mpaka sasa hajaonyesha makeke Jangwani.
Ingawa Diego amefunga bao moja pekee katika ligi tangu asajiliwe ameshindwa kuonyesha vitu vyake kwa Pluijm na kuushawishi uongozi na mashabiki jambo ambalo linamuweka kwenye wakati mgumu na kwa mujibu wa watu wa ndani ya uongozi lolote linaweza kutokea hasa Yanga ikiingia kwenye makundi Afrika.
Klabu ikiingia kwenye makundi inaruhusiwa kusajili mchezaji mpya kwa ajili ya kuongeza nguvu hata kama atakuwa hakucheza ligi ya ndani. Ili mradi klabu anayotoka isiwe bado kwenye mashindano hayo makubwa ya Afrika.
Baadhi ya viongozi wanadai mchezaji huyo maarufu kama Diego alivamiwa na malaria ikamtoa mchezoni, lakini itamtumia muda mrefu kuwa fiti wakati Yanga inahitaji watu wa kazi wa haraka.
“Ni wachezaji wazuri sana wamenivutia kuna vitu kidogo wanakosa, lakini nimevutiwa nao jinsi walivyocheza mechi hii nitawaangalia zaidi katika mchezo wa marudiano nafikiri tunatakiwa kuwa nao makini na ni wachezaji ambao kocha yeyote anaweza kuwa nao,” alisema Pluijm.
“Yule namba 11 (Sibomana) alikuwa hatari sana ukiangalia alikuwa anapiga krosi nyingi zenye madhara hasa katika kipindi cha pili ambacho hatukucheza katika ubora wetu.”
ATAKA MABAO 67
Akizungumzia kasi ya ufungaji katika kikosi chake Pluijm alisema mpaka sasa Yanga imeshafunga mabao 51 katika Ligi Kuu na matano katika Ligi ya Mabingwa, lakini kwake ni mabao machache kulingana na nafasi wanazotengeneza.
Raia huyo ya Uholanzi alisema mpaka sasa Yanga ilitakiwa iwe na jumla ya mabao yasiyopungua 67 ikiwa ni idadi ndogo kulingana na nafasi wanazotengeneza jambo ambalo bado ataendelea kuwasisitizia umakini wachezaji wake.
“Yanga ndiyo timu inayotengeneza nafasi nyingi sasa ubora wa namna hiyo ni lazima uendane na ufungaji si sahihi mpaka sasa kufunga mabao 51 pekee, tulitakiwa kufanya vizuri zaidi,” alisema Pluijm.

0 comments:
Post a Comment