KIUNGO mshambuliaji wa Mbeya City Fc, Haruna Moshi amesikitishwa na matokeo ya sare ambayo timu yake iliyapata juzi jumamosi kwenye mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Akizungumza na mbeyacityfc.com, Haruna ambaye pia anajulikana kwa jina la Boban alisema kuwa kabla ya mchezo huo kila kitu kilikuwa sawa upande wao kama wachezaji na kila mmoja alikuwa na ari ya kutaka kushinda ili kupata pointi tatu muhimu ambazo zineisogeza City kwenye nafasi nyingine katika msimamo wa ligi hiyo.
“Tulijiandaa vizuri kushinda mchezo huo, ari ilikuwa kubwa, kabla mwalimu alitueleza juu ya kucheza kwa nidhamu ili kuepuka kadi zisizo na maana,makosa madogo yalitugharimu tukafungwa bao la mapema na wakati tunajipanga kukaa vizuri wapinzani wetu walipata penalti, hakika bao la pili lilituchanganya zaidi”alisema.
Akiendelea zaidi Boban ambaye kabla ya kujiunga na City alikuwa mchezaji wa Simba na Coastal Union aliweka wazi kuwa alilazimika kuvaa majukumu ya nahodha wake Hassani Mwasapili kuwatuliza wachezaji wenzake uwanjani ili watulie na kupanga mashambulizi upya kutafuta mabo ya kusawazisha na ushindi.
“Mwasapili alikuwa nahodha uwanjani, baada ya kufungwa bao la pili nilimfuata na kumwambia azungumze na wenzangu, kwa sababu tushafungwa tutulie ili tuweze kurudisha na kutafuta ushindi lakini akaniomba mimi nifanye hivyo, nashukuru mungu bada ya hilo mambo yakaenda sawa kila mmoja akarudi mchezo na tukafanikiwa kupata bao moja kabla ya mapumziko”
Baada ya mapumziko na kurudi kipindi cha pili City ilibadiri mchezo na kuanza kucheza pasi fupi fupi za haraka huku akiwatumia zaidi walinzi wa pembeni kupiga krosi za mwisho, ilifanya hivyo muda mwingi kabla ya Issa Nelson aliyeingia kipindi cha pili kufunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Boban.
“Kwenye vyumba vya mapumziko mwalimu alituambia tubadiri mchezo,akawaingiza vijana wenye uwezo wa kukimbia na mpira, yalikuwa nimabadiliko yenye tija kubwa, nashukuru tukafanikiwa kufunga bao la pili, hili lilituongezea nguvu na kucheza zaidi lakini hatukuweza kubadili kitu baada ya hapo”, alisema Boban akimaanisha kumalizika sare ya 2-2 baada ya dakika 90 za mchezo huo.
“Nimesikitishwa na matokeo haya, si yale tuliyoyatarajia lakini sina njia nyingine zaidi ya kukubaliana nayo kwa sababu hii ni soka na matokeo hayo yapo, kikubwa tunajipanga upya kuhakikisha tunapata matokeo kwenye mchezo unaofuata kabla hatujaenda Dar es Salaam kucheza na Young Africans”,alimaliza.

0 comments:
Post a Comment