Mabingwa wa soka Tanzania bara, Dar Young Africans kesho watacheza mechi ya tatu ya kirafiki katika kambi yao ya Mbeya ambapo watachuana na Wagonga nyundo wa Mbeya City FC.
Mchezo huo unaotarajia kuwa kipimo kizuri kwa kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm na City, Juma Mwambusi utaanza saa 10:00 jioni ndani ya dimba la Sokoine, jijini Mbeya.
Hata hivyo, katika mechi nne walizokutana katika misimu miwili, Mbeya City haijawahi kuifunga Yanga.
Msimu wa 2013/2014 kwenye uwanja wa Sokoine, City walitoka sare ya 1-0 na wakafungwa 1-0 mechi ya pili uwanja wa Taifa.
Msimu uliopita, City walikubali kichapo cha 3-1 katika mechi zote mbili.
Kiingilio cha mtanange huo ni shilingi za Kitanzania Elfu nne ( 4,000/=).
Mpaka sasa Yanga wamecheza mechi mbili mkoani humo na kushinda zote.
Mechi ya kwanza walishinda 4-1 dhidi ya Kimondo FC, wafungaji wakiwa ni Geofrey Mwashiuya (mawili), Amissi Tambwe na Simon Msuva,
Mchezo wa pili walishinda 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons.
Malim Busungu na Amissi Tambwe ndio walicheka na nyavu katika kipute hicho kilichojaa ubabe, huku mlinzi wa kushoto wa Yanga, Mwinyi Hajji akioneshwa kadi nyekundu.
Agoti 22 mwaka huu, Yanga watacheza na Azam FC katika mechi ya Ngao ya Jamii uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, ikiwa ni kuashiria ufunguzi wa msimu wa 2015/2016 wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Yanga wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa penati 5-3 na Azam katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Kagame lililomalizika mapema mwezi huu kwa Azam kutwaa ubingwa wao wa kwanza.


0 comments:
Post a Comment