Baada ya mapumziko ya siku tatu, Wekundu wa Msimbazi Simba
kesho jioni wanatarajia kuanza mazoezi ikiwa ni muendelezo wa kujiwinda na
michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara inayotarajia kuanza Septemba 12 mwaka
huu.
Mkuu wa Idara ya habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Haji
Sunday Manara amesema kikosi chao kipo
sawasawa kuanza matizi, ingawa mpaka muda huu hajui watatumia uwanja upi.
“Kesho jioni tunaanza mazoezi, sijajua ni uwanja gani,
lakini nitakufahamisha baadaye”. Amesema Manara.
Agosti 8 mwaka huu ambayo ni siku ya Simba, vijana wa Muingereza, Dylan Kerr walishinda
1-0 dhidi ya Sports Club Villa ya Uganda katika mechi ya kimataifa ya kirafiki
iliyopigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Goli pekee la ushindi lilifungwa na Awadh Issa Juma dakika
ya 90 ya mchezo.
Mnyama Simba hajawahi kutwaa ubingwa tangu alipofanya hivyo
msimu wa 2011/2012 na kuelekea msimu mpya wa 2015/2016, benchi la ufundi,
viongozi, wachezaji, wanachama na mashabiki wake wana matumaini ya kurejesha
heshima.
Hata hivyo, watakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa
mabingwa wa kandanda Tanzania bara, Dar Young Africans na miamba ya kandanda Afrika
Mashariki na kati, Azam FC ambao toka msimu wa 2012/2013 wanachuana nafasi
mbili za juu.


0 comments:
Post a Comment