Hatma ya Elius Maguri na Ivo Mapunda bado haijajulikana ndani ya klabu ya Simba, huku kila mchezaji akiwa na mazingira tofauti ya ama kuendelea kusalia kwenye klabu hiyo au kutokuwepo kabisa msimu ujao wa ligi kuu Tanzania bara 2015-2016.
Rais wa Simba SC, Evans Aveva ameweka wazi kuwa hatma ya Maguri iko mikononi mwa kamati ya usajili ya klabu hiyo kufuatia kocha Dylan Kerr kumuengua katika kikosi chake kilichocheza mechi ya Simba Day dhidi ya SC Villa.
Kuhusiana na Ivo, Aveva amesema klabu yake inasubiri pande hizo mbili kukutana na kutiliana saini.
“Elius Maguri jina lake halikuwepo kwa vigezo ambavyo mwalimu anavijua na sisi kama wanasimba na ‘stake holders’ wa mpira, siku zote mmekuwa mkiwapigia kelele viongozi hasa wa vilabu vya Simba na Yanga kwamba tumekuwa tukiingilia majukumu ya walimu, sisi tukaona tuheshimu hilo pamoja na kwamba Maguri tulimsajili kwa matumaini makubwa”, amesema Evans Aveva
“Lakini mwalimu alipokuja akaona uwezo wa Maguri ni mdogo kwa hiyo katika ile mechi ya Villa akaona asishiriki, kinachofuata baada ya hapo ni maongezi pamoja na viongozi wa Simba kujua hatma yake.
Zaidikuhusu Ivo, Aveva amefafanua kuwa, mazungumzo yameshafanyika na imebaki kutiliana.
“Ivo Mapunda ataendelea kuwa mchezaji wa Simba Sports Club katika kipindi kinachokuja”.
“Mazungumzo yalifikia hitimisho na wakakubaliana, Ivo atakuja kusaini mkataba na klabu yetu ya Simba, mpaka hivi ninavyozungumza ni kwamba ni bahati usajili umesogezwa mbele, kwa hiyo bado tuna muda lakini mpaka hapa ninavyozungumza Ivo bado hajaonekana kuja kusaini mkataba Simba, hivyo jukumu hili limerudishwa tena katika kamati husika na Ivo bado yupo Dar tutatoa majibu”.


0 comments:
Post a Comment