Manji (katikati) akiwasi kwenye ofisi ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ambazo mtandao huu umezipata zinaeleza kwamba jina la Mwenyekiti wa Yanga Yusuf Manji inasemekana limeenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania Udiwani Kata ya Mbagala Kuu.
Vyanzo vinaeleza kuwepo kwa mchezo mchafu ‘figisufigisu’ katika ‘kulikata’ jina lake, wakati alishinda kwa kishindo kwenye kura za maoni akiomba kuteuliwa na chama chake cha CCM kugombea nafasi hiyo .
Manji (katikati) akiingia kwenye lango la ofisi za Mkoa
Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) leo walijazana kwenye ofisi ya chama hicho mkoa wa Dar es Salaam wakisemekana kukipinga kuenguliwa kwa Manji, huku wakitaka ufafanuzi wa kina juu ya sababu zilizotumika kuliondoa jina lake mpendwa wao.
Hata hivyo mpaka sasa Chama Cha CCM hakijatoa tamko juu ya sakata hilo.
Wanachama wa CCM ambao ni wakazi wa kata ya Mbagala Kuu wakiwa kwenye ofisi za chama hicho mkoa wa Dar es Salaam wakisemekana kusubiri hatma ya Manji
Baada ya muda mfupi tangu mtandao huu upige kambi yake kwenye Ofsi ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Manji akiwa katika hali ya udhoofu aliwasili akiwa na bahasha mkononi inayosemekana ni barua ya kupinga maamuzi ya kuliondoa jina lake kwenye kinyang’anyiro hicho.
Mtandao huu ulijaribu kufanya mazungumzo na Manji lakini alidai hayuko katika hali yake ya kawaida kutokana na kusumbuliwa na maradhi hivyo hayupo tayari kuzungumza chochote kwa muda huo na kuomba akimilishe kile kilichompeleka kwenye ofisi za CMM Mkoa.
Baada ya zoezi la kuzungumza na Manji kukwama, mtandao huu ukaona ni vyema kuzungumza na baadhi ya wanachama ambao walikuwa wamepiga kambi kwenye ofisi hizo kusubiri hatma ya mgombea wanaedai ndiye chaguo lao.
Victor Chitete amehusisha kukatwa kwa jina la manji na siasa za Simba na Yanga kutokana na baadhi ya viopngozi wa juu wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam kuwa ni mashabiki, wanachama na wanazi wa Simba ambao ni watani wa jadi wa Yanga.
“Kuna viongozi wa nafasi za juu kwenye chama ngazi ya mkoa ambao wanafanya kila liwezekanalo ili kuzuia Manji asipite kwenye nafasi ya Udiwani anayogombea kwasababu ya siasa za Simba na Yanga kwasababu wao ni viongozi wa klabu ya Simba”.
Shabani Dotto Kadala yeye ni mwanachama wa CCM na mkazi wa Kata ya Mbagala Kuu amesema, Manji ni mtu makini na wanaimani nae kutokana na uwezo wake aliouonesha wa kuiongoza klabu ya Yanga yenye mamilioni ya washabiki na kumudu kuiongoza kwa utulivu bila migogoro kama ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.
“Manji ni mtu makini na ni mtekelezaji, amethibitisha hilo akiwa Yanga. Ninavyoiangalia Yanga haina mjadala kwamba Manji ni mchapakazi na ni mtendaji. Ameweza kutoa ajira nyingi kupitia Yanga wengine wakiwa ni wadogozetu. Kupitia hilo sisi hatuna mashaka nae”, amesema Kadala.
“Tumekuja kufikisha ujumbe kwamba tunamuhitaji mgombea wetu bwana Yusuf Manji ambaye tulimpitisha kwenye kura za maoni na kuna tetesi kwamba jina lake limekatwa. Taarifa hizi tumezipata kwa viongozi wetu na baadhi ya wanachama wa CCM wa Mbagala Kuu, walitueleza kwamba kiongozi wetu jina lake limekatwa”.
“Tumefika hapa katibu mwenezi wa mkoa wa Dar es Salaam ametuhakikishia kuwa jina la Manji limekatwa na ametupa sababu kadhaa ambazo wanadai hakuwahi kuhudhuria kwenye baadhi ya vikao vya kuomba kura za maoni na kutangaza kura zake. Wanadai viongozi wa Kata na Wilaya walimuita hakufika kitu ambacho si kweli. Sisi wanachama tulionananae akatueleza sera zake tukavutiwa nazo tuka mchagua”.
0 comments:
Post a Comment