Kikosi cha Azam FC
Michuano ya Kombe la Kagame inayoendelea kutimua vumbi jijini Dar es salaam, leo inaingia katika siku ya nne kwa kuwakutanisha Matajiri wa Dar es salaam, Azam FC dhidi ya Malakia kutoka Sudani Kusini, mchezo utakochezwa katika uwanja wa Taifa majira ya saa 10 kamili jioni.
Mchezo wa kwanza unaoanza majira ya saa 8 kamili mchana uwanja wa Taifa utazikutanisha timu za Al Shandy ya Sudan dhidi ya LLB ya Burundi, huku uwanja wa Karume majira ya saa 10 kamili jioni Heegan FC ya Somalia wakionyeshana ubavu dhidi ya APR kutoka Rwanda.
Jumatano kutakuwa na michezo mitatu ambapo mchezo wa kwanza uwanja wa Taifa utawakutanisha Khartoum ya Sudan dhidi ya KMKM ya Zanzibar saa 8 mchana, huku uwanja wa Karume saa 10 jioni KCCA ya Uganda wakiwakaribisha Adama City kutoka Ethiopia.
Katika uwanja wa Taifa jumatano saa 10 jioni, Telecom ya Djibout watakuwa wenyeji wa Yanga SC ambayo kocha wake mkuu Hans Van Der Pluijm ameahidi kupata ushindi katika mchezo huo.
Hans amesema mchezo wa ufunguzi dhidi ya Gor Mahia walipoteza kutokana na kucheza pungufu kwa takribani dakika 60, hivyo anawaandaa vijana wake kufanya vizuri siku ya jumatano na kuwapa furaha wanachama na wapenzi wa Yanga SC.

KHATROUM, GOR MAHIA ZASHINDA
Mabingwa mara tano wa michuano ya Kombe la Vilabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati timu ya Gor Mahia kutoka nchini Kenya, jana wameshinda mchezo wake wa pili mfululizo baada ya kuichapa KMKM ya Visiwani Zanzibar kwa mabao 3-1.
Mabao ya Gor Mahia yalifungwa na mshambuliaji Meddy Kagere bao moja, Michael Olunga aliyefunga mabao 2, huku bao la kufutia machozi la KMKM likifungwa na Matheo Anthony.
Katika mchezo wa awali uliochezwa saa 8 mchana, Khartoum ya Sudan iliichapa timu ya Telecom ya Djibout kwa mabao 5- 0, mabao ya Khartoum yalifungwa na Wagdi Abdallah, Ousmaila Baba, Murwan Abdallah, na Salah Bilal aliyefunga mabao mawili.
Kwa matokeo hayo ya jana Gor Mahia wamefikisha pointi 6, wakifuatiwa na Khartoum yenye pointi tatu sawa na KMKM wakipishana kwa idadi ya magoli ya kufunga na kufungwa.
0 comments:
Post a Comment