Supastaa wa zamani wa Barcelona, Ronaldinho 'Gaucho' ametambulishwa rasmi mbele ya maelfu ya mashabiki wa klabu ya Fluminense wakielekea kucheza mechi ya watani wa jadi dhidi ya Vasco Da Gama kwenye uwanja wa Maracana, Brazil.
Mshindhi huyo mara mbili wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa FIFA (2004, 2005) ambaye amesaini klabu hiyo ya Brazil akiwa mchezaji huru, amepokelewa kishujaa uwanjani na kupewa jezi yake ya heshima, namba 10.
Ronaldinho aliripotiwa kwamba angetua Uturuki majira haya ya kiangazi baada ya kumalizana na klabu ya Queretaro ya Mexixo, lakini kiungo huyo mshambuliaji ameeleza sababu za kurudi Brazil.
"Natamani kuweka historia katika klabu hii." Amesema Ronaldinho wakati wa kutambulishwa.
"Kilichonishawishi mimi ni kukosa ubingwa wowote wa Brazil. Imenishawishi sana. Hii ni klabu kubwa yenye wachezaji wakubwa, tuna kila kitu cha kutufanya kuwa mabingwa"
Ronaldinho mwenye miaka 35, alianza kucheza mpira katika timu yake ya nyumbani ya Club Gremio ya Mjini Porto Alegre kabla ya kwenda Ulaya ambako alizichezea Paris Saint Germain, Barcelona na AC Milan.
Pia alirejea Brazil kuichezea Flamengo na baadaye akaijiunga na Atletico Mineiro ambapo alitwaa kombe la klabu bingwa America Kusini, ' Copa Libertadores' mwaka 2013.
Mashabiki wa soka Duniani kote wanafurahi kuona fundi mkubwa wa soka kuwahi kutokea Duniani bado anaendelea kucheza na hana mpango kwa kustaafu.

0 comments:
Post a Comment