Na Mwandishi wetu
Katika sehemu ya pili ya habari hii kuhusu upangaji matokeo unavyolitafuna sola la Tanzania jana, tuliona jinsi matukio ya upangaji matokeo yameachwa bila kuadhibiwa licha ya kuwapo kwa ushahidi wa vitendo hivyo.
Leo tunawaletea sehemu ya tatu ya mfululizo wa habari hii ya kiuchunguzi juu ya kadhia hiyo. Sasa endelea.
TFF KUTOADHIBU NYOTA YANGA
Wadau wa soka waliohojiwa na gazeti hili pia walidai TFF imekuwa na utaratibu wa kutochuku hatua dhidi ya baadhi ya klabu pindi zinapokiuka kanuni, taratibu na katiba ya shirikisho hilo.
Masau Bwire, msemaji wa klabu ya Ruvu Shooting, alisema alishangazwa na kitendo cha TFF kutomchukulia hatua stahiki mshambuliaji wa Yanga kutoka Burundi, Amissi Tambwe, kutokana na nyota huyo wa zamani wa Simba na klabu ya Vital'O ya Burundi kumdhalilisha beki wa kati wa Simba, Mganda Juuko Murshid.
Katika mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2014/15 iliyomalizika kwa Wanamsimbazi kushinda 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Machi 8, Tambwe alimvuta sehemu za siri beki huyo, kitendo ambacho ni kinyume cha Ibara ya 11(f) cha Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012.
"Msimu huu (2014/15) beki wetu George Michael alifungiwa mechi tatu na TFF kutokana na kumkaba koo Tambwe wakati wa mechi yetu dhidi ya Yanga iliyomalizika kwa suluhu kwenye Uwanja wa Taifa. Tambwe amefanya udhalilishaji dhidi ya mchezaji wa Simba, lakini hajaadhibiwa na TFF. Je, Kanuni za Nidhamu za TFF haziwahusu wachezaji wa Yanga?" Alihoji Bwire.
CANNAVARO AMDHALILISHA ASKARI POLISI
Mbali na Tambwe, TFF haikuchukua hatua dhidi ya nyota kadhaa wa Yanga waliofanya makosa ya utovu wa nidhamu msimu uliopita akiwamo nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro' aliyemdhalilisha askari polisi wa kike uwanjani.
Februari 4, Cannavaro (pichani) alifanya kitendo cha udhalilishaji kwa kumkumbatia na kumpiga mabusu askari polisi mwanamke aliyekuwa na sare za Jeshi la Polisi Tanzania wakati beki huyo akishangilia bao lake alilofunga katika dakika ya 11 ya mechi waliyoshinda 1-0 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, kinyume cha Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012.
Kamati ya Nidhamu ya TFF ilikutana jijini Dar es Salaam Februari 5 na kuwaadhibu Juma Nyosso wa Mbeya City FC na Aggrey Morris wa Azam FC kutokana na makosa mbalimbali huku ikiacha kumwadhibu Cannavaro.
Nyosso, mchezaji wa zamani wa Simba na Coastal Union, alifungiwa mechi nane kutokana na kumdhalilisha mshambuliaji Elias Maguri wa Simba kwa kupenyeza kidole cha kati kwenye makalio wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo City ilishinda 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa Januari 28.
Morris alifungiwa mechi tatu za ligi hiyo kutokana na kumpiga kiwiko makusudi kiungo mshambuliaji wa Simba kutoka Uganda, Emmanuel Okwi, wakati timu hizo zilipochuana na kutoka sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa Januari 25.
Kwa mantiki hiyo, adhabu dhidi ya Morris ilitoka siku 11 baada ya beki huyo kumpiga Okwi wakati ile ya Nyosso ilitoka siku nane baada ya nyota huyo wa City kumdhalilisha Maguri, lakini shirikisho hilo bado halijatoa hukumu ya kumfungia Tambwe mechi nane kutokana na kumdhalilisha Murshid kwenye Uwanja wa Taifa Machi 8 mwaka huu kwa mujibu wa Ibara ya 11(f) cha Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012.
Aidha, Januari 22 Kamati ya Waamuzi ya TFF kupitia kwa mwenyekiti wake, Saloum Chama, ilitangaza kumfungia refa wa kati Teofile ikiwa ni saa chache baada ya Yanga kutishia kutopeleka timu uwanjani kwa madai kuwa refa huyo wa Morogoro aliachia Tambwe akabwe koo na beki wa kati wa Ruvu Shooting, Michael katika mechi yao ya Januari 18. Hukumu hiyo ilitoka siku nne baada ya mechi kati ya timu hizo.
KAULI YA TFF
Alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia suala la Tambwe, Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa, alisema tayari wameshamfungulia kesi katika Kamati ya Nidhamu ya shirikisho hilo.
"Kuna mtu anaweza kuiba leo, akafikishwa mahakamani na kuhukumiwa siku hiyo hiyo, lakini mtu mwingine anaiba leo na anakamatwa na kufunguliwa kesi, lakini anakaa rumande baada ya miezi mitatu hukumu yake ndiyo inatoka.
"Kamati ya Nidhamu ya TFF ni kamati huru, kwa hiyo panaweza kuwa na sababu. Pengine aliitwa na hakuhudhuria au kuna mambo yanayochunguzwa. Kama Tambwe asingekuwa amefunguliwa kesi, basi ningesema wamefumbia macho," alisema.
Kuhusu udhalilishaji uliofanywa na Cannavaro dhidi ya askari polisi wa kike jijini Tanga, Mwesigwa alisema maofisa wa TFF waliokuwa wamepangwa kusimamia mechi ya Coastal dhidi ya Yanga hawakuripoti tukio hilo katika ofisi yake.
"Kamati inayohusika (Kamati ya Nidhamu ya TFF) haikuletewa ripoti ya suala hilo. Ofisi yangu haiwezi kuwasilisha kesi ambayo haina ushahidi ndiyo maana hata watu wa Simba wana imani na mimi, licha ya kwamba nimefanya kazi Yanga nikiwa katibu mkuu wa klabu," alisema Mwesigwa.
Kutoadhibiwa kwa Cannavaro na Tambwe licha ya kufanya vitendo hivyo vya utovu wa nidhamu, kulikuwa na faida kubwa kwa kikosi cha Yanga katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.
Katika mechi zote nane alizocheza baada ya kumdhalilisha Murshid Machi 8, Tambwe alifunga mabao 11 yaliyoipa timu yake pointi zote 24 na kurahisisha kazi kwa Wanajangwani kupata taji la 25 la Tanzania Bara.
Mechi hizo ni zile walizoshinda 2-1 dhidi ya Kagera Sugar Machi 18 (alifunga bao moja), 2-0 dhidi ya Mgambo Shooting Machi 21 (alifunga bao moja), 3-1 dhidi ya JKT Ruvu Machi 25 (hakufunga), 8-0 dhidi ya Coastal Union Aprili 8 (alifunga mabao manne), 3-1 dhidi ya Mbeya City Aprili 12 (hakufunga), 3-2 dhidi ya Stand United Aprili 21 (alifunga bao moja), 5-0 dhidi ya Ruvu Shooting Aprili 24 (alifunga bao moja) na 4-1 dhidi ya Police Moro Aprili 27 (alifunga mabao matatu).
Katika mechi nane ambazo Cannavaro alipaswa kufungiwa kwa kumdhalilisha askari polisi wa kike Februari 4, Cannavaro, beki wa kati na Nahodha wa Taifa Stars, alifunga bao moja huku safu ya ulinzi ya Yanga ikiruhusu kufungwa mabao manne.
Mechi hizo walishinda 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Februari 8, 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons Februari 19, 3-1 dhidi ya Mbeya City Februari 22, wakafungwa bao 1-0 dhidi ya Simba Machi 8 kisha wakashinda 2-1 dhidi ya Kagera Sugar Machi 18, 2-0 dhidi ya Mgambo Shooting Machi 21, 3-1 dhidi ya JKT Ruvu Machi 25 na 8-0 dhidi ya Coastal Union Aprili 8.
CHANZO: MTANDAO WA IPP MEDIA
0 comments:
Post a Comment