![]() |
Abdallah Kibadeni |
KOCHA wa zamani wa Simba, Alhaj Abdallah Kibadeni 'King Mputa' ameshangazwa na kitendo cha bodi ya ligi na wadhamini wa ligi kuu soka Tanzania bara, Vodacom, kumpa tuzo ya ukocha bora Mbwana Makata ambaye aliinusuru timu kushuka daraja badala ya kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm aliyeipa timu ubingwa.
Winga huyo wa zamani wa Simba ambaye anashikilia rekodi ya kufunga magoli matatu peke yake 'Hat-trick' kwenye mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga mwaka 1977 amesema kocha aliyeipa timu mafanikio ndiye anayestahili kuchukua tuzo hiyo.
"Hili suala la kuchagua kocha bora nashindwa kuelewa wanatumia kigezo gani, bora maana yake kizuri, kitu kinachopendeza, lakini kama kocha bora anatoka timu ya mwisho inayonusurika kushuka daraja mimi sielewi. Unamuondoa mtu aliyechukua timu na akachukua ubingwa mimi sielewei, labda wanaangalia uzawa, lakini hata yule aliyechukua ubingwa mbona ana msaidizi wake? kwanini asichukue yeye (Charles Mkwasa)." Amesema Kibadeni ambaye aliifikisha Simba fainali ya kombe la CAF mwaka 1993 siku hizi kombe la Shirikisho.
"Kama walitoa zawadi kwa mtu aliyeinusuru timu iliyotaka kupotea kuliko yule aliyechukua ubingwa, mimi sikubaliani nao kwamba kocha bora atokane na timu inayonusurika kushuka na si yule anayeisaidia timu kupata mafanikio. Tunamkatisha tamaa, kila mtu atahangaika tu, labda wangeweka zawadi mbili".
Mbali na Pluijm, Makata alikuwa akishindana na aliyekuwa kocha wa Simba, Goran Kopunovic.
Msimu wa 2012/2013, Kibadeni aliiwezesha Kagera Sugar kumaliza nafasi ya nne na kuteuliwa kuwa kocha bora wa VPL.
2013/2014, kocha bora alikuwa Juma Mwambusi baada ya kuisaidia Mbeya City kushika nafasi ya tatu, lakini mwaka huu hakutajwa hata kwenye orodha ya wanaowania tuzo.
0 comments:
Post a Comment