ETOILE du Sahel wanaikaribisha Yanga katika mechi ya
marudiano ya hatua ya 16 bora ya kombe la Shirikisho inayopigwa kesho mjini
Sousse Tunisia kuanzia saa 3:00 usiku kwa saa za Tanzania.
Mabingwa wa Tanzania, Yanga, wanahitaji ushindi wa aina
yoyote ile au sare ya angalau magoli 2-2 ili kusonga mbele moja kwa moja. Hii
inatokana na sare ya 1-1 waliyopata uwanja wa Taifa, Dar es salaam majuma
mawili yaliyopita.
Kuelekea katika mechi hiyo, MPENJA BLOG imezungumza na mchezaji wa zamani wa Yanga ambaye kwa
sasa ni kocha wa mpira wa miguu na mchambuzi wa soka katika kituo cha Azam TV, Ally
Mayay Tembele akieleza mbinu ambazo Yanga wanatakiwa kutumia ili kuwashinda
Etoile.
Mayay ameanza kwa kufafanua kuwa mpango wa mechi (Game Plan)
huanzia nje ya uwanja na unapoingia uwanjani unakwenda kutekeleza tu.
“kwanza kwa nje ya uwanja nafasi kubwa ni saikolojia, kama
timu unajiandaa na kufanyiwa vibaya ‘Fitina’ kuanzia hotelini, unapoingia
uwanjani na sehemu yoyote ile”. Amesema Mayay na kusisitiza: “ Mazingira
hayawezi kuwa rafiki, ukiona mtu anakutendea vibaya unatakiwa kujiandaa
kufunga, unajua kabisa kwamba kesho mimi nitafunga, kwa mfano walikaa karibia saa
tatu uwanja wa ndege, sio suala la kulalamika, ni suala la kujiandaa”
Beki huyo na kiungo wa zamani wa Yanga ameeleza mbinu za
uwanjani ambazo Wanajangwani wanatakiwa kuzitumia ili kuwamaliza Waarabu.
“Ukifika uwanjani kwenye mechi kubwa kama hiyo unatakiwa
kujiandaa kucheza mpira, ukisema unakwenda kukaba utapata matatizo, siku zote
ukiwaruhusu wao wacheze mpira maana yake watakushambulia muda wote na
ukishambuliwa kwa muda mrefu uwezekano wa kufanya makosa ni mkubwa, kwahiyo
utafungwa tu”
YANGA WAFANYEJE SASA?
Mayay anasema: “Kikubwa ni kuhakikisha wanamiliki mpira, uliona
katika mechi ya kwanza hapa nyumbani, kipindi cha kwanza waliwaruhusu Waarabu
watengeneze nafasi nyingi sana ingawa hawakuwa makini sana wale Etoile du
Sahel, kama wangekuwa makini wangepata mabao matatu”
“Yanga wategemea kuwa watashambuliwa kutoka dakika ya kwanza
mpaka ya mwisho, njia sahihi ya kujilinda ni kukaa na mpira, angalau umiliki
uwe asilimia 50 kwa 50, usiache wamiliki mpira wao kwasababu utakuwa unakaba
muda wote”.
KIUNGO FUNDI HARUNA NIYONZIMA HAYUPO KWENYE MECHI HIYO
KUTOKANA NA KADI TATU ZA NJANO, JE ITAATHIRI TIMU?
Mayay anajibu: “Haruna (Niyonzima) hatakuwepo leo, ni
mchezaji ambaye ana umuhimu pale timu inapotaka kucheza mpira, sio mtu muoga,
kuna wakati mechi inakuwa ngumu na viungo wanashindwa kucheza kwa mfano akikaa
na mpira mara ya kwanza akaharibu hataki kwenda kuomba, lakini Haruna ni mtu
anayefanya kazi, lazima kutakuwa na pengo”
“Yanga wana watu wanaoweza kuifanya kazi nzuri, wanaweza
wasiwe wabunifu sana kama Haruna kwasababu anakaa na mpira na anasaidia kiungo,
Telela (Salum) hayuko fiti kwasababau hajacheza, lakini kutokana na uzoefu wake
wa kucheza Yanga na baadhi ya mechi za kimataifa anaweza kucheza vizuri ingawa
si kwa kiwango cha juu”.
NANI MWINGINE ANAWEZA KUFANYA KAZI NZURI SAFU YA KIUNGO?
Mayay anafafanua: “Wapo baadhi ya watu kama Said Juma, kama
atapewa nafasi anaweza kucheza mpira, inawezekana katikati pasiwe na ubunifu,
lakini kikubwa ni kumiliki mpira, mwalimu anaweza kuweka washambuliaji watatu,
Kpah Sherman, Mrisho Ngassa pamoja na Msuva au hata Tegete, Mrwanda ambao
wamekwenda. Katikati kuna akina Makapu (Said Juma), Telela (Salum), Mbuyu
(Twite) au hata Zahir (Rajab) akacheza kama kiungo mkabaji na wakaongeza nguvu
kwasababu katikati licha ya kuhitaji ubunifu pia panahitaji nguvu”.
Kila la kheru Yanga katika mechi yenu!!
0 comments:
Post a Comment