Na Baraka Adson Mpenja
Mtazangazi wa Mpira wa miguu, Azam TV
Tel:0712461976
YANGA imetupwa nje ya michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika na Etoile du Sahel ya Tunisia kwa ushindi wa jumla wa magoli 2-1.
Mtazangazi wa Mpira wa miguu, Azam TV
Tel:0712461976
YANGA imetupwa nje ya michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika na Etoile du Sahel ya Tunisia kwa ushindi wa jumla wa magoli 2-1.
Mechi ya kwanza iliyopigwa majuma mawili yaliyopita uwanja wa Taifa Dar es salaam, Yanga na Etoile walitoka sare ya 1-1 na jana usiku Wanajangwani walifungwa goli 1-0 mjini Sousse, Tunisia.
Etoile sasa watacheza na moja ya timu zitakazotolewa ligi ya mabingwa barani Afrika kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho.
Goli la Etoile jana lilifungwa na Ammar Jemal dakika ya 24 akimalizia krosi ya Alkhali Bangoura.
Kwa yeyote aliyetazama mechi ya jana hususani kipindi cha pili lazima akubaliane na ukweli kwamba Yanga walicheza vizuri.
Licha ya mapungufu yaliyojitokeza katika safu ya ulinzi kutokana na kukosekana kwa kamanda Nadir Haroub 'Cannavaro' na Niyonzima sehemu ya kiungo, Yanga walijitahidi kuisogeza timu mbele na kutengeneza nafasi kadhaa.
Salum Telela alicheza vizuri licha ya kutokuwa fiti asilimia 100 na alitolewa dakika ya 82, nafasi yake kuchukuliwa na Andrey Coutinho.
Kwa ujumla wake, Yanga kama timu walifanya kazi nzuri, vipaji binafsi pia vilionekana kuisaidia timu.
Kitu kikubwa nilichokiona jana ni Yanga kucheza bila uoga, walifunguka, walikaba vizuri, walitengeneza nafasi, lakini walishindwa kuzitumia. Kama Amissi Tambwe na Kpha Sherman wangekuwa makini wangeweza kushinda.
Matokeo ya sare ya 1-1 nyumbani yamewaharibia Yanga, wangeweza kushinda mechi, lakini wakiwa uwanja wa Taifa walicheza kwa tahadhari, hofu na walishindwa kujiamini tofauti na jana ambapo walicheza kwa kiwango cha juu.
Ilifika wakati Etoile waligundua mechi imekuwa ngumu, walichokuwa wanakifanya ni kuzozana na wachezaji wa Yanga mara kwa mara, hii ilidhihirisha mechi ni ngumu kwao.
Lakini kwa upande mwingine hizi ni 'janja janja' za kupoteza muda, waligundua hawawezi kuongeza goli tena kirahisi, hivyo wakawa wanalazimisha kuzozana na kufanya vurugu za uwanjani kwa maana mbili, moja kupoteza muda na pili kuwaondoa mchezoni Yanga.
Hii ni kawaida kwa timu za kiarabu wanapocheza nyumbani na kiukweli jana kadi nyekundu aliyopata Frank Kom dakika ya 42 baada ya kuoneshwa kadi mbili za njano, moja akimchezea vibaya Mrisho Ngassa na ya pili akimchezea madhambi Simon Msuva iliwasaidia sana Yanga ingawa walishindwa kupata goli.
Ni mara chache sana timu za kiarabu kupapa kadi nyekundu nyumbani dhidi ya timu za Afrika mashariki, lakini ya jana imedhihirisha kuwa mechi ilikuwa upande wa Yanga.
Safari moja huanzisha nyingine, Yanga wameshatolewa na sasa wanaanza maisha mengine ya ligi kuu wakiwa tayari ni mabingwa.
Mwakani wanarudi tena kucheza ligi ya mabingwa barani Afrika na ili kufika mbali wanatakiwa kufanya yafuatayo:
Mosi, kuiandaa timu kwa muda mrefu. Yanga wanahitaji kuwa na fikra za kimataifa, waiandae timu kwa mashindano hayo. Moja ya matatizo ya klabu za Tanzania ni kuanzia pale walipoishia.
Mwaka huu timu inaweza kufanya vizuri, mwakani ikatolewa mapema zaidi. Hii inatokana na kukosa utashi wa kujua wanataka nini, timu ikitolewa hatua ya 16 bora, inabidi ifikirie kuzidi hatua hiyo mwakani? je Yanga watafika mbali zaidi mwakani wakicheza ligi ya mabingwa? inategemeana na utashi wa viongozi wao.
Pili; naamini kuna haja ya kuongeza baadhi ya wachezaji katika safu zote, hawa waliopo ni wazuri, lakini kuna kitu kinakosekana kwa wachezaji waliowengi yaani uzoefu wa michuano mikubwa ya kimataifa.
Wanaweza kuwa wamecheza michuano ya kimataifa, lakini ni kwa ngazi ipi?, walifika wapi?, ndio maana kuna haja ya kutafuta wachezaji wa kiwango cha juu waliowahi kufika zaidi ya 16 bora.
Hili linawezekana kama Hans van Pluijm ataachiwa kazi ya kusajili. Kuna wachezaji Afrika magharibi na kaskazini mwa Afrika wanaoweza kuisaidia Yanga, tatizo ni mfumo wa kuwapata.
Kwasababu wanakwenda kushindana na timu kubwa mwakani, mabingwa wa nchi mbalimbali, wanatakiwa kujiandaa kuongeza nguvu katika kikosi chao. Waongezwe wachezaji wenye uzoefu mkubwa na mashindano ya klabu bimgwa.
Tatu; wasilewe sifa za kijinga, kuna msemo mmoja unawafanya watu wajisahau, eti wamekufa kiume, katika mpira wa miguu hakuna kufa kiume.
Mbona Yanga walimiliki zaidi mpira kipindi cha pili, lakini hawajasonga mbele? kitu chenye maana zaidi kwenye michezo ya mtoano na ligi kuu ni goli. Kucheza sana hakuna maana yoyote, ndio maana unaona Jose Mourinho anaweza kupaki basi lakini akapata matokeo na leo hii anatarajia kutangaza ubingwa wa EPL na Chelsea yake.
Yanga wanatakiwa kuachana na sifa za kitoto, wanahitaji kujiandaa mara tu watakaporudi Dar es salaam, mpira ni mchakato, unahitaji muda, maandalizi ya saikoloji, kutengeneza muunganiko wa timu, vyote hivyo vinatengenezwa kwa muda mrefu.
Uwepo mfumo mzuri wa kuendelea kuisuka timu kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kufikia mwakani timu iwe tayari. Itakuwa ajabu sana kama wachezaji wataendelea kuwa walewale na mawazo yaleyale ya viongozi.
Lazima waangalia makosa yamefanyika wapi, udhaifu uko wapi ili waboreshe. Wanaweza kuwabakiza wachezaji wote, lakini kuongeza wengine wa ngazi ya juu ni jambo la muhimu zaidi.
Ikumbukwe kuwa waliofanikiwa katika soka walifeli sana. Kushindwa ni changamoto. Pluijm anaweza kuendelea na hao hao ili kuwafanya wakae pamoja muda mrefu zaidi, lakini ukimuuliza hata kesho atakwambia anahitaji kusajili wachezaji ili kuboresha maeneo kadhaa ya timu.
Viongozi wa Yanga msikilizeni 'Babu' Pluijm anataka nini, fanyieni kazi, fikirieni kimataifa zaidi, wekeni mikakati ya muda mrefu, mwakani mnaweza kufika mbali.
Jumapili njema!
Maoni: 0712461976
0 comments:
Post a Comment