WAKATI imeripotiwa kwamba rais wa Burundi, Piere Nkurunziza
ametua jana mjini Bujumburu kutoka Dar es salaam Tanzania, hali ya utulivu
imeanza kurudi nchini humo.
Jana Nkurunziza ali-tweet akithibitisha kurejea nchini kwake
na kuwashukuru wanajeshi watiifu na polisi kwa uvumilivu wao wa kuipigania
serikali iliyopo madarakani.
Mkuu wa jeshi la Burundi
amesema jaribio la mapinduzi lililofanywa na Jenerali Godefroid Niyombare
halijafanikiwa.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi na Yanga, Amissi Tambwe
aliyepo eneo la Akamba nchini humo kwa mapumziko baada ya ligi kuu soka
Tanzania bara kumalizika mei 9 mwaka huu, amezungumza na mtandao huu kueleza
hali ya mambo inavyokwenda.
“ Mambo yametulia, televisheni ya taifa inaonesha vipindi
vya kawaida kama kawaida. Serikali ya mwanzo bado ipo madarakani na ndio ilizua
hizo vurugu, lakini sahizi mambo shwari, hakuna vurugu tena”. Amesema Tambwe na
kufafanua: “Mchezo wa soka unakutanisha watu, unawaweka watu pamoja na kuleta
amani, shughuli za mpira zinaendelea, wakati nakuja jana (juzi) nimepita maeneo
kadhaa na kuona watu wanaendelea kucheza kama kawaida”.
Tambwe ameshika nafasi ya pili kwa ufungaji wa magoli (mabao
14) msimu wa 2014/2015 nyuma ya mfungaji bora wa msimu wa 2014/2015 aliyetikisa
nyavu mara 17, Simon Msuva.
Msimu wa 2013/2014, Tambwe akiichezea Simba aliibuka
mfungaji bora kwa kutikisha nyavu mara 19 na anatajwa kuwa mshambuliaji hatari
zaidi kwa misimu miwili mfululizo.
0 comments:
Post a Comment