MOJA ya stori kubwa kwasasa nchini Tanzania ni kitendo cha
kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa kusaini
mkataba wa miaka minne (4) kuichezea klabu ya Free State Stars inayoshiriki
ligi kuu nchini Afrika kusini.
Mkataba huo mnono umesainiwa jana ‘Bondeni’ baada ya pande
zote mbili kufikia makubaliano.
Mtandao huu umefanya jitihada za kumtafuta Ngassa na kufanya
naye mahojiano maalumu;
Swali: Umekuwa na safari ndefu ya kutafuta timu nje ya
nchi na wakati mwingine ulizitosa ofa, pia ulishindwa kufuzu majaribio kama
ilivyotokea West Ham na kwingineko, lakini sasa umesaini Free Stars Stars,
unasikiaje kufikia mafanikio hayo?
Ngassa: Kwanza kabisa
namshukuru mwenyezi Mungu kwasababu malengo ambayo niliyapanga naona yanaanza
kutimia, najisikia vizuri.
Swali: Umesaini mkataba mrefu wa miaka minne, ina maana
utacheza kwa kipindi chote klabuni hapo au kuna kipengele kinachoruhusu kuuzwa
timu nyingine?
Ngassa: Mkataba wangu wa
miaka minne sio kwamba nitamaliza yote hapa hapa, hapana!, kama itatokea timu
nyingine labda ikafika ofa, wanaweza kuniuza, kuna kipengele kinachoeleza kuwa kama
timu nyingine inaweza kutokea naweza kuuzwa.
Swali: Mapokezi yakoje?
Ngassa: Namshukuru Mungu, mapokezi
ni mazuri sana!
Swali: Baada ya kusaini mkataba utaendelea kuwepo Afrika
kusini au utarudi kwanza nyumbani Tanzania?
Ngassa: Leo nitaungana na
timu ya taifa (Taifa Stars), nitaenda Hotelini ambapo watafikia.
Swali: Wewe ni mtu wa familia, je utaiacha familia yako
Tanzania?
Ngassa: Kwa mkataba
niliosaini natakiwa kuja na familia, kweli nashukuru Mwenyezi Mungu.
Swali: Kwa mafanikio uliyofikia, bila shaka kuna watu wengi
wamechangia, lakini ni akina nani ambao huwezi kuwasahau?
Ngassa: Nashukuru timu zote nilizoweza kupita hadi
kufikia hapa. Nimeanza safari ndefu toka nikiwa mdogo, kuna watu wengi wametoa
mchango wao mpaka kufikia hapa, kwahiyo nashukuru timu niliyoanzia ya Toto
Africans, nikaja Kagera Sugar, nikaja Yanga, nikaenda Azam na baadaye nikaenda
Simba na baadaye nikarudi Yanga ambako nimeweza kupata ubingwa, namshukuru
mwenyezi mungu kwa yote hayo.
Swali: Kucheza soka la kulipwa katika ligi kubwa ya Afrika
kusini maana yake umekuwa nembo ya Tanzania, utatumiaje nafasi hiyo kupeperusha
bendera ya nchi yako na kuwa chachu ya wengine waliopo nyuma yako kuja huko?
Ngassa: Kikubwa najua
nawakilisha nchi yangu ya Tanzania, najua nawatangaza ambao wako nyuma yangu
kama walivyofanya waliopita mfano huku alipita Nteze John, pia kama ilivyo kwa
akina Samatta (Mbwana) waliopo nje, ikitokea nafasi nyingine nitasapoti
watanzania wengine waje, mtu kama Simon (Msuva), Mkude (Jonas) au Domayo
(Frank) na wengine ili tuweze kuungana labda timu moja.
Swali: Free State Stars wameanza kuiwinda saini yako kwa muda
gani?
Ngassa: Hawa jamaa toka
tunacheza Challenge Uganda walikuwa wananifuatilia, walishaongea sana na Yusuf (Bakhresa)
nikiwa Azam, tena kipindi hicho ikaja ofa nyingine ya El Merreikh, walianza
kunifuatilia toka zamani sana pamoja na Bocco (John).


0 comments:
Post a Comment