Perez (kulia) amemfukuza Carlo Ancelotti
Wachezaji wake wametoa madukuduku yao. Wanataka
Carlo aendelee kuwafundisha. Vivyo hivyo kwa mashabiki, kupitia vyombo vya
habari jijini Madrid, walisema wanataka aendelee kuwepo. Watu wa Bernabeu
wamekuwa waaminifu, mara chache sana wamekuwa waaminifu hivi linapokuja suala
hili. Wanapenda wawe naye tena msimu ujao. Yeye (Ancelotti) pia hapendi kuondoka.
Sasa
ni kwa nini Ancelotti si kocha wa Real Madrid tena?
Hili ni swali
ambalo halina utani hata kidogo. Unapoulizwa swali kama hili, wengine wanaweza
kusema ni kwa sababu ya Barcelona. Baada ya ‘kutoka kapa’ msimu huu. Sio
tu kwamba Barcelona wameshinda La Liga, huku kukiwa na uwezekano wakushinda
makombe matatu msimu huu – lakini pia wamekuwa gumzo tena kwa watu wapenda soka
kutokana na jinsi wanavyotandaza soka la uhakika.
Hiyo ni kitu hatari kwa kocha yeyote
atakayechaguliwa na Rais wa Madrid kukutana nayo. Unaweza kuwa ulihisi hili,
Florentino asingeweza kukubali hali hii. Sio kwamba, Perez anataka Real ishinde
makombe makubwa tu lakini pia anataka timu yake iwe tishio balaa kama
ilivyokuwa kipindi akiwa kijana mdogo.
Kipindi cha kina Alfredo Di Stefano, Ferenc Puskas,
Francisco Gento na Jose Santamaria. Kipindi ambacho watu walikuwa wakiwaangalia
wanaume kumi na moja wakiwa kwenye jezi zao nyeupe, wakiwafanyia ‘maangamizi ya kutisha’ timu pinzani, sio
tu kuwa na mafanikio na klabu kutisha sokoni. Perez anataka Real Madrid itawale
kila mahali lakini utawala uanzie uwanjani.
Kwa hiyo Barcelona inaposhinda makombe. Ni kitu
kibaya. Lakini Barca ilipomchukua Neymar kabla yake (kitu ambacho hadi leo bado
kinamuumiza), ni jambo lingine baya. Lakini yote hayo tisa, linapokuja suala la
Lionel Messi, Neymar, na Suarez kuwa ni utatu unaotisha zaidi duniani basi hapo
Perez anazidi ‘kuvurugwa’.
Hebu tuyaweke hayo yote katika upande mmoja kwa
muda.
Ni kweli Ancelotti ameondolewa kwa sababu timu yake
ilishinda makombe manne tu katika misimu miwili? Inawezekana. Kushinda La Liga
au Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya sio tiketi ya moja kwa moja kuendelea kuwa
kocha wa Real. Muulize Jupp Heynckes, muulize Vicente Del Bosque: watu
waliotemwa na Perez lakini wakaja kutisha sana baada ya kuondoka.
Kikosi cha Ancelotti kilitakiwa kiwe angalau
kimeshinda La Liga mara moja, au mara zote mbili wakati akikiongoza. Lakini
tujikumbushe jinsi alivyoshinda makombe yake manne. Barcelona ilifungwa kwenye fainali
ya Kombe la Mfalme. Atletico huku wakidhani wameshashinda Ligi ya Mabingwa,
ghafla walijikuta wakishushiwa ‘mvua’
ya magoli kwenye mechi ya fainali.
Ushindi wa 2-1 kwenye Super Cup ya Ulaya ambayo huwa
ni mechi moja tu, waliifunga Sevilla. Kilikuwa ni kisasi kizuri kwa sababu
Sevilla waliwaharibia kampeni yao ya kushinda La Liga.
Je waliifunga moja ya timu kubwa wakati wanashinda
Kombe la Dunia kwa Vilabu? Hapana. Lakini kuwa bingwa wa dunia inatia moyo sana
na inawafanya wachezaji wawe vema kisaikolojia.
Kwa makombe hayo aliyoyashinda, je alijua ni lazima
ashinde La Liga au kibarua chake kitaota nyasi?
Napenda kujua jibu lake, lakini nadhani jibu ni
hapana. Kusema kwamba kushinda taji hilo kungemfanya awe salama moja kwa moja.
Kushinda tena Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya
ingekuwa ni jambo la kihistoria. Haijawahi kufanyika kabla (kwa utaratibu huu
wa sasa). Lakini ni ubabe uliopitiliza
kusema kwa kocha aliye katika msimu wake wa pili, afanye jambo ambalo hakuna
aliyeweza kulifanya kabla au anafukuzwa.
Kwa hiyo wakati Ancelotti akielekea kwenye mwaka
wake wa sabato (sabbatical year – hii ni kulingana na alivyosema mwenyewe). Je
ni taji la La Liga ndilo lililomgharimu? Inawezekana kabisa.
Hakuna kipindi ambacho tungeweza kusema kwamba Real
Madrid imeshashinda La Liga lakini kuna kipindi ilionekana kuwa na nguvu sana.
Kusema kweli ilijichanganya yenyewe na kuliachia kombe hili, ndio maana
Barcelona – nayo ambayo kuna kipindi hali ya ndani ya klabu haikua shwari –
iliweza kurudi kwenye kampeni na kushinda.
Kipindi ambacho Ancelotti aliadhibiwa zaidi ni kile
kipindi kilichozidi mwezi kati ya siku za mwanzoni za mwezi Februari hadi
katikati ya mwezi Machi. Kipindi hiki kilikuwa kibaya zaidi kwa zama za hivi
karibuni za klabu hiyo.
Vipigo – ‘dhahama’
iliyowashukia Calderon – kutoka kwa Atletico, Athletic, Barcelona na Schalke,
droo ya nyumbani dhidi ya Villareal. Hali ya kujiamini ilipotea na kulikuwa
hamna njia sahihi (kutosha) ya kutatua matatizo yaliyokuwa yanawakabili.
Hicho ndicho kipindi ambacho Madrid walipoteza taji
hilo na Ancelotti kupoteza kazi yake.
Kama Real wangepata sare dhidi ya Atleti na
Athletic, na kuifunga Barcelona (ambayo walionekana wanaweza katika kipindi cha
kwanza pale Camp Nou) na kupata pointi zote tatu dhid ya Villareal. Wangekuwa
mabingwa sasa hivi. Hata sare tatu za ugenini na ushindi nyumbani bado ingeweza
kuwapa ubingwa.
Makosa tena yalionekana kwenye mechi dhidi ya
Juventus, hasahasa kushindwa kupata ushindi kwenye mechi ya pili. Madrid haikuwa na nguvu, fiti, makini,
haikuweza kushambulia na pia ilikosa stamina. Walianza kuonekana kama Barca
ilivyokuwa msimu uliopita.
Tatizo lingine kubwa ilikuwa hali ya kujirudia rudia
ya majeruhi kwa wachezaji. Chanzo kinaweza kuwa mipango yao ya uimara kwa
wchezaji (fitness strategy) inakosa baadhi ya vitu au mazoezi yao ya kila siku
hayafanywi kwa usahihi.
Lakini – hapa ndipo boss Perez anatakiwa kuwa makini
zaidi – Barcelona wameonesha msimu huu kwamba hilo linaweza kusahihishwa.
Mchanganyiko wa Ubora namaandalizi sahihi ya mazoezi, mzunguko (rotation) bora
wa wachezaji wa kiwango cha juu.
Madrid inabidi iangalie nini kimewazunguka.
Wameshinda kombe moja la La Liga katika misimu saba iliyopita, wameshinda
makombe mawili ya Ligi ya Mabingwa, mataji matatu ya La Liga na mawili ya Kombe
la Mfalme katika miaka 12 ya Perez kama Rais wao. Wanadhihakiwa kwa hayo pia.
Kama wakiangalia pembeni yao – sio tu kwa Barcelona
bali Sevilla na Atletico pia – kwa nini Perez hajifunzi kuwa, njia ya kuelekea
mafanikio na makombe zaidi ni aidha kuwa na kanuni moja inayoendana na DNA ya
klabu au kumweka mtu mmoja, awe kocha kwa kipindi kirefu (kama Monchi kwa
Sevilla) ili kuhakikisha kwamba mawimbi hayasababishi Meli kuzama hata pale
hali ya hewa inapobadilika.
Atletico wao wameweza kushinda makombe mawili ya
Ligi ya Europa, moja la Mfalme na moja la La Liga katika misimu mitano
iliyopita. Hayo ni matunda yaliyotokana na mmiliki wao, Miguel Angel Gil,
ambaye anawaamini wakurugenzi bora wa mpira, wamwongoze. Ataandika kile
anachokitaka, aina ya mpira ambao wadhamini na mashabiki watalipa ili
kuungalia, pia atapanga ukomo wa bajeti.
Sevilla imekuwa ni klabu inayojiendesha yenyewe
tangu mwaka 2000, ya Ramon “Monchi” Rodriguez. Ameitengenezea klabu hela nyingi
na kuendeleza mfumo mzuri wa kuendeleza
vijana, na ushindi wa Sevilla kwenye Ligi ya Europa (Europa League) jana usiku
kunamaanisha hilo limekuwa kombe lao kubwa la sita katika miaka tisa (bila
kuhesabu Super cup za Spain). Kuwa makini Florentino.
Na hatimaye, Barcelona. Mafanikio yao yametokana na
Johan Cruyff aliyeona amedharauliwa kuuzwa Real Madrid bila ruhusa yake mwaka
1973, na kulazimisha kuuzwa Camp Nou, badala yake. Baada ya kurudi kwake kwa
mara ya pili kwenye klabu (kama kocha) tangu 1989 mpaka sasa klabu imeweza
kufikia maono yake, kwa kufanya miaka 25 iliyopita kuwa miaka yao yenye
mafanikio na kuvutia zaidi katika historia. Hii ndio klabu inayomnyima usingizi
Florentino, lakini bado hajifunzi kwao.
Carlo Ancelotti angesikilizwa ili atoe mwongozo wa
nani asajiliwe nani aachwe atemwe, na nani auzwe.
Lakini je kumuondoa Ancelotti kutaponya matatizo ya
Real Madrid? Hapana. Kwa sababu tatizo kubwa la Real Madrid, hata pale mambo
yanapokuwa mazuri, linabaki kuwa moja tu, nalo ni Florentino Perez. Yeye ni
maji na petroli kwenye tanki lao la mafuta.
0 comments:
Post a Comment