Ni vita kali kati ya timu yenye mafanikio zaidi
Italia dhidi ya taasisi inayojiita “zaidi
ya klabu” – lakini timu hizi, Juventus na Barcelona, zitacheza fainali ya
Ligi ya Mabingwa mwaka huu jijini Berlin zikiwa na alama tofauti za kujivunia.
Miaka tisa iliyopita, Juventus ilikuwa ikicheza
katika Serie B (Daraja la chini baada ya lile la Ligi Kuu ya Italia) baada ya
kuadhibiwa kutokana na kuhusika kwao katika kashfa ya upangaji matokeo (Calciopoli
scandal). Wachezaji kama Gigi Buffon, Claudio Marchisio na Giorgio Chiellini
walikwepo wakati timu ikiwa Serie B na sasa watakwepo katika mechi ya fainali,
Berlin, Juni 6, hawa wamekwepo tangu klabu ilipoanguka hadi kuzaliwa upya.
Wachezaji hawa wataingia kwenye mechi hiyo wakiwa na kumbukumbu za kusota
kwenye ‘joto la jiwe’ hadi sasa
wakiwa ‘ matawi ya juu’
Msimu wa 2006 – 07, Lionel Messi, Xavi na Andres
Iniesta walikuwa wakiichezea Barcelona kipindi hicho ikiwa ni mabingwa watetezi
wa taji la Ligi ya Mabingwa wakati wenzao, Juve, walikuwa wakicheza dhidi ya timu kama Cittadella na Crotone. Hii
itakuwa fainali ya tatu ya Barcelona tangu msimu ule, ikiwa ni baada ya
kushinda fainali ya 2009 na 2011, baadhi ya mashabiki wa Barcelona
wanaamini kama sio ‘mbinu chafu’ za
Inter ya Mourinho 2010, na ‘basi la
Chelsea’ 2012, basi hii ingekuwa fainali yao ya tano ndani ya miaka saba.
Hakuna swali la nani ataingia kama mbabe kwenye
fainali hii. Juventus itaingia kama ‘wanyonge’
(underdogs) uwanjani, hili ni jambo ambalo wao hawajalizoea kwa nafasi yao.
Barcelona inapewa nafasi kubwa hasa kutokana na uchezaji wao na namna
walivyofuzu kucheza fainali hii.
Barca itaingia ikiwa na kikosi chao cha ‘mauaji’ kikiwa na utatu unaoonekana
kuwa mkali zaidi kuwahi kutokea katika uso wa dunia – Messi, Luis Suarez na
Neymar wamefunga jumla ya magoli 121 kati yao katika msimu huu – hii ikiwa ni
tangu Alfredo Di Stefano, Paco Gento na Ferenc Puskas waongoze safu ya
ushambuliaji ya Real Madrid.
Kikosi cha Luis Enrique kimetengenezwa na wachezaji
waliozoea kushinda na wanaocheza kulingana na utamaduni wa Barca, wachezaji
ambao ‘hawatishwi na hali yoyote’
katika mechi kubwa zaidi kwa ngazi ya vilabu duniani. Kama kutakuwa na hali
yoyote ya ‘kwikwi’ basi hiyo itakuwa
kwa wachezaji wapya kama Luis Suarez, Marc-Andre ter Stegen na Ivan Rakitic.
Lakini, tuache ukweli usemwe, hilo halionekani kutokea hasa kutokana na
muunganiko wao katika timu.
Juventus, yenyewe imejengwa na maveterani
pamoja na vijana wawili wakali walioonekana hawafai katika vilabu vyao vya
zamani: Alvaro Morata na Paul Pogba. Ambao wameshashinda medali kadhaa kama
watu binafsi. Carlos Tevez, Patrice Evra, Andrea Pirlo, Morata na Buffon wote
wameshacheza fainali ya Ligi ya Mabingwa hapo nyuma. Tofauti yao sasa ukilinganisha
na Barca ni kuwa wameweza kufikia fainali hii wakicheza pamoja kwa umoja kama
timu wakati hapo zamani waliweza kufika katika fainali huku wakiwa na wachezaji
wenye majina makubwa.
Tofauti nyingine kati yao na Barcelona ni hii,
wakati kikosi cha Barca kikionekana kitaendelea kuwa pamoja na kusonga mbele,
hilo haliwezi kuongelewa kwa Juve ambayo wachezaji wao kadhaa wamekuwa
wakitakiwa na vilabu vingine vikubwa barani Ulaya. Jaribu kupeleka akili yako
mbele misimu mitatu ijayo, ukiondoa wachezaji kama Dani Alves na labda Javier
Mascherano na Iniesta (japo ni kama haiwezekani) wachezaji wao wote wanaweza
kuendelea kuwa pamoja Camp Nou.
Kwa bianconeri
haiko hivyo. Real Madrid wana nafasi
ya kumnunua tena (buy-back option) Morata
huku Pogba akitazamiwa kuwa ‘bidhaa
inayohitajika zaidi sokoni’ wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa,
Juve kuzuia uhamisho wake haitakuwa rahisi.
Pia tukija kwenye suala lingine la umri, Tevez ana
miaka 31 na hajawahi kuficha matamanio
yake ya kumalizia soka lake nyumbani kwao, Argentina. Buffon ana miaka
38, Pirlo 35, Evra 33 na Stephan Lichtsteiner ana miaka 31. Kwa namna yeyote
ile, timu hii inahitaji kufanyiwa marekebisho angalau: ni vizuri kwao kupunguza
baadhi ya wachezaji hawa wakati huu ambao bado viwango vyao vipo juu kabla
nafasi hiyo haijapotea.
Tukiachana na vigezo vyote vya kiufundi
tulivyoviongelea hapo juu, upinzani mwingine wa aina yake katika fainali hii huu hapa. Suarez atakutana
uso kwa uso na wabaya wake wa hapo nyuma katika nyakati tofauti, Evra na
Giorgio Chiellini. Huku katikati ya uwanja kukiwa na ‘vita’ ya aina yake kati ya ‘mafundi’
wawili wenye vipaji vya hai ya juu, Andres Iniesta dhidi ya Andrea Pirlo.
Pia hali nyingine ya kiushindani itakuwa kati ya Neymar
na Pogba, ambao wamepishana miezi 11 tu katika kuzaliwa kwao, hawa wanatazamiwa
kushika jukwaa la ushindani wa nani bora duniani baada ya zama za Cristiano
Ronaldo na Lionel Messi kupita.
Buffon na Pirlo wanarudi kwenye uwanja ule ule
walionyanyua Kombe la Dunia mwaka 2006.
Unahitaji stori zaidi? Tevez atacheza dhidi ya Messi ikiwa hata
mwaka haujapita tangu fainali ya Kombe la Dunia, Brazil ichezwe ambayo
walitakiwa waongoze safu ya ushambuliaji ya Argentina pamoja, lakini Tevez
aliishia kuangalia fainali ile kwenye televisheni kwa sababu aliachwa kwenye
kikosi cha Argentina.
Hii ndio Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya,
itakayokuja kwako tarehe 6 mwezi wa 6. Tunza tarehe hii.
0 comments:
Post a Comment