Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Azam imeambulia sare ya 1-1 katika mechi mbili zilizopita dhidi ya City na Mtibwa.'
KIKOSI cha Azam FC kinachowakosa washambuliaji Kipre Tchetche na Khamis Mcha pamoja na beki wa kati Aggrey Morris, kimetamba kufanya vizuri dhidi ya Mgambo Shooting Stars katika mechi pekee ya kesho ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayochezzwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Jaffar Idd Maganga, msemaji wa Azam FC, ameuambia mtandao huu akiwa jijini Tanga leo mchana kuwa licha ya kuwakosa nyota hao, kikosi chao kimejiandaa vyema kuhakikisha kinashinda na kufufua matumaini ya kutetea taji lao la ligi hiyo.
"Tunashukuru Mungu tulifika salama hapa Tanga. Tchetche, Aggrey na Mcha hawakusafiri na timu kutokana na matatizo ya kifya," amesema.
Tchetche, mchezaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita na mfungaji bora wa ligi hiyo msimu wa 2012/13, anasumbuliwa na malaria, Morris aliumia enka wakati Mcha amefungwa plasta ngumu kutokana na kupata majeraha ya mguu wakati wakijiandaa kwa mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar FC.
Kuelekea mechi ya kesho, Bakari Shime, kocha mkuu wa Mgambo Shooting Stars, amesema kuwa anatambua mechi itakuwa ngumu kutokana na ubora wa kikosi cha Azam, lakini wamejiandaa kushinda nyumbani.
Mgambo na Azam hazijawahi kucheza hata mechi moja msimu huu kutokana na kufinyangwa finyangwa kwa ratiba ya ligi hiyo kunakofanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Wanalambalamba wamepata sare ya 1-1 katika mechi mbili zilizopita dhidi ya City na Mtibwa wakati Mgambo ilifungwa 2-0 na Yanga SC kabla ya kushinda 4-0 dhidi ya Polisi Moro FC katika mechi mbili zilizopita jijini Tanga.


0 comments:
Post a Comment