Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Loga aliwahi kuwa kocha mkuu wa Gor Mahia ya Kenya na Simba ya Tanzania.'
Kocha mkuu wa AFC Leopards, Zdravko Logarusic 'Loga' amesema mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) bado ni mbichi na ubingwa uko wazi kwa kila timu inayoshiriki ligi hiyo.
Baada ya raundi ya sita ya KPL, Ingwe, timu ya Loga, iko nafasi ya nane, pointi nne nyuma ya vinara na wapinzani wao wakubwa Gor ambao pia wana mechi moja mkononi, lakini licha ya kuwa na mwanzo mbaya, Loga amesema ubingwa wa KPL bado uko wazi huku akiahidi kupindua msimamo ulivyo na kufanya kweli katika ligi hiyo.
Logarusic pia ameweka wazi kwamba anahitaji wiki tatu za kuwakimbiza wachezaji wa timu yake mpya ili wawe fiti.
Marathon
"Hii ni (ubingwa) ni marathon, bado mapema kujua nani atakuwa bingwa katika hatua hii ya mwanzo na ubingwa uko wazi kwa kila timu. Timu zote zitakumbana na changamoto mbalimbali wakati ligi inaendelea. Kwa sasa ninachohitaji ni wiki tatu za mazoezi magumu kuhakikisha nyota wangu wanakuwa fiti," amesema Loga.
Logarusic ameanza kuinoa klabu hiyo mwanzo mwa msimu huu akitokea kwao Croatia alikokuwa huru baada ya kutimuliwa Simba siku chache kabla ya msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuanza.


0 comments:
Post a Comment