Simba waligoma kuingia vyumbani kwenye mechi dhidi ya Mbeya City jumamosi ya juma liliopita na kufungwa 2-0
Na
Shaffih Dauda
MTANDAO
huu kwa muda mrefu sasa umekuwa ukifanya tafiti na kufuatilia mwenendo wa klabu
ya Simba katika mechi za ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu.
Mwishoni
mwa juma lililopita, Simba ilifungwa magoli 2-0 na Mbeya City fc katika uwanja
wa Sokoine, Mbeya na kuifanya klabu hiyo kongwe nchini kuendelea kukaa nafasi
ya tatu kwa pointi 35 walizokusanya baada ya kushuka dimbani mara 22.
Machi 18
mwaka huu walifungwa magoli 2-0 na Mgambo JKT katika uwanja wa CCM Mkwakwani
Tanga, lakini wakashinda 2-1 ugenini dhidi ya Kagera Sugar uwanja wa CCM
Kambarage, Shinyanga na ilikuwa aprili 6 mwaka huu (jumatatu ya pasaka).
Katika
mechi hizo tatu, mtandao huu ulikuwa unachunguza mwenendo wa Simba na namna
wanavyoiandaa timu kwa ajili ya mechi.
Katika
mechi ya Tanga waliyochapwa na Mgambo, timu iligoma kuingia kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo, wachezaji wakakaguliwa ndani ya basi nje ya geti karibu na
vyumba vya kubadilishia nguo.
Simba
walifanya hivyo wakihofia kurogwa na wenyeji wao, lakini mwisho wa siku wakafa
mbili bila na walipoenda Shinyanga kucheza na Kagera walifanya hivyo hivyo,
walikataa kuingia vyumbani na kukubali kutozwa faini na TFF.
Simba waliendeleza
tabia yao ya kutoingia vyumbani kwa madai ya kuogopa kurogwa huku wakisingizia
vyumba ni vibovu. Inawezekana kweli ni vibovu, lakini dhahiri walikuwa na
mawazo mengine kichwani mwao kwani viongozi walionekana kuwapangia wachezaji
maeneo ya kupita wakati wanaingia uwanjani.
Baada ya
safari ndefu ya uchunguzi, hatimaye jibu limepatikana kule Mbeya ambako Simba
amekufa tena mbele ya Wagonga nyundo wa Mbeya, Mbeya City fc.
Tulipiga
kambi jijini Mbeya na kugundua kuwa Simba wameharibikiwa kwasababu wanawatumia
Waganga wa kienyeji kwa muda mwingi wakiamini watawasaidia kupata matokeo ndani
ya uwanja.
Dunia ya
leo klabu kongwe ya Simba, mfano wa kuigwa inaendekeza imani za kishirikina kwa
kiwango cha juu namna hii, inasikitisha sana.
Chakusikitisha
zaidi ni kwamba, tunaamini viongozi waliopo madarakani ni vijana wa kidijitali
yaani wa kisasa au kileo. Imefika wakati tunaamini wazee kama vile Hassan
Dalali na wengineo hizi si zama zao, lakini hayo ni maneno tu, inawezekana wale
wazee wakawa na mafanikio makubwa kuliko
vijana ambao tunaamini wanaweza kuiendesha timu kileo au kisasa, vijana
ambao ukiwaangalia ni watanashati, lakini matendo wanayoifanyia klabu ni mabaya
mno.
Kwa aina
ya viongozi wa sasa wa Simba, ni jambo la aibu kutumia muda mwingi kuwekeza
katika uchawi , kutumia waganga au ndumba wakiamini watasaidia kupata matokeo
kuliko kujikita katika maandalizi ya kitaalamu na kiuweledi.
Simba wamefungwa
na Mbeya City kwasababu hawakutoa nafasi ya kiuweledi katika maandalizi yao,
waliwekeza nguvu kwa mambo ya nje ya uwanja wakiamini yatawasaidia kupata
matokeo.
Mbeya City walicheza vizuri
Utaratibu
ulivyo, unapoenda uwanja wa ugenini, siku moja kabla ya mechi, timu inatakiwa kufanya mazoezi kwenye uwanja
ambao watachezea mchezo, kwahiyo Simba walitakiwa kwenda kufanya mazoezi Sokoine
siku ya ijumaa, lakini kutokana na kuamini mambo ya kishirikina hawakwenda
kufanya mazoezi siku hiyo, matokeo yake ilibidi wafanye mazoezi kwenye bustani
(Garden) ya Hoteli waliyofikia, wanafanyia mazoezi ‘Garden’ eti kwa sababu
wanaogopa kurogwa na Mbeya City.
Hii
ilikuwa kinyume, mwalimu na benchi la ufundi walitaka timu ikafanye mazoezi
uwanjani, lakini baadhi ya viongozi walioandama na timu waliona timu ikienda
kufanya mazoezi Sokoine wataenda kupoteza mchezo wa jumamosi.
Mwisho
wa siku wakafanya mazoezi uani, wakafanya mazoezi ‘Garden’, na wakawa ‘wamefeli’
rasmi.
Ikaja
siku ya mechi, badala ya kupita kwenye mlango wa kawaida wakapitia mlango wa
nyuma, wachezaji wakashuka na kuingilia mlango wa nyuma, wakashindwa kuingia kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo, wakakaa pembeni kwenye kona kulia kwa jukwaa kuu la Sokoine,
sehemu ambayo maaskari Polisi wanapenda kuweka magari yao.
Baadaye
kidogo wakaenda karibu na sehemu ya vyumba vya kubadilishia nguo na kukaa nje
upande wa kulia kwenye chumba chao , lakini wachezaji wakaamuriwa waondoke tena.
Muda huo
wachezaji wa Mbeya City walikuwa wanapasha moto misuli ‘Warm-up) na walikuwa
wameshafanya kwa muda mrefu, Simba wao walichelewa hata kupasha moto misuli kutokana
na mambo yao ya kishirikina.
Wakati
wanaingia kwenye ‘Warm-up’ badala ya kuingilia kwenye benchi ambalo watakaa
upande wa kushoto kwasababu kulia walikuwa wamekaa Mbeya City kinyume na
taratibu zinazowataka wenyeji kukaa benchi la kushoto na wageni kulia, Simba wakarudi
kwenye kona waliyoingilia mara ya kwanza
Simba
walifuata taratibu kwamba wenyeji wanakaa benchi la kushoto, wageni kulia,
lakini kulia ni sehemu ambayo Mbeya City wanakaa kila siku na Simba walikataa
kukaa kushoto wakiamini pameshapigwa misumari. Walipotaka kukaa kulia Mbeya
City wakagoma na ndipo ikatokea vurumai kati ya watu wa Mbeya City na Simba,
ikabidi Simba wawe wapole na kukubali kukaa kushoto.
Wakati
huo wachezaji walikuwa wamekaa chini nyuma ya lile benchi la ufundi na ilibidi wakafanye
‘warm-up’, kwa itikadi hizo hizo za kishirikiana wakashindwa kuingia uwanjani
kupitia eneo hilo, wakaambiwa watembee na kurudi goli la kusini wazunguke kwenye
kibendera cha kona na waingie uwanjani na mstari ule wakafanye ‘warm-up’.
Ukiangalia
kwa undani, wachezaji hawataki mambo
hayo, wanakasirika, wanaingia uwanjani hawana raha, lakini kwasababu
wamelazimishwa na wapambe wanaojifanya wanajua kila kitu, timu iingilie wapi, wakanyage wapi na
kamwe hawataki kukiuka maigizo ya waganda wa kienyeji.
Siku ya
mechi hakika wachezaji hawakuwa sawa kisaikolojia, waliingia kupasha misuli na
kuanza mechi, wakati wanacheza Mbeya City waliwazidi Simba, walikuwa
wamechangamka, walionesha kabisa wanahitaji matokeo, lakini Simba walikuwa wanacheza
tu kama vile mtu anayetaka kutekeleza jukumu lake na kuondoka.
Jonas
Mkude, Abdi Hassan Banda, Said Ndemla wakawa wanazunguka tu, wanageuka nyuma na
mipira, hawaoneshi nia ya kwenda mbele, Elius Maguli, Ibrahim Hajibu
wakaonekana vimeo kwasababu walikuwa hawapati huduma kutoka kwa viungo.
Mbeya City
walicheza vizuri sana ukiachana na mambo ya kupiga misumari kwa wale wanaoamini
hivyo, lakini kwasisi ambao hatuamini hivyo, tukiamini kuwa maandalizi ya mechi
ni mazoezi, Mbeya City walicheza zaidi ya Simba, walitengeneza nafasi nyingi na
kilichosababisha Simba washindwe kucheza ni imani za kishirikina.
Kuna
baadhi ya wachezaji ambao sitaki kuwataja hawafurahishwi na vitendo vya
kuendekeza vitendo vya kishirikina, walienda Tanga kuchuana na Mgambo, kuna mtu
mmoja wa kamati ya utendaji (jina tunalo) anapenda sana mambo ya kishirikina,
alienda na waganga karibia nane (8) Mkwakwani, wakapigwa 2-0 na Mgambo.
Pointi
yetu ni kuwakanya Simba na timu nyingine za ligi kuu kuachana na mambo ya
kuamini waganga . Hata tabia ya Mbeya City kulinda uwanja, kuchimbua uwanja na
kufukia vitu ni ya kishamba, matokeo hayapatikani kwa njia ya Waganda. Mbona
kuna mataifa yanasifika kwa uchawi lakini wanaboronga katika soka?
Hata
hapa Tanzania maeneo yanayosifika kwa uchawi mfano Sumbawanga mbona hawana hata
timu ya ligi kuu?
Inawezekana
waganda wanatumika kwasababu ya mila na desturi za kizamani, lakini hayatakiwi
kufanyika kwa kasi ya ajabu kama wanavyofanya Simba na timu nyingine.
Kama
yanafanyika kwasababu za kitamaduni basi yafanyike kwa siri pasipokuwahusisha
wachezaji, haiwezekani eti wamekuja waganga usiku Hotelini, wachezaji
wanaamushwa usiku kusikiliza maelekezo ya Waganga.
Unawachosha
wachezaji, hawapumuziki vizuri, matokeo yake wanapoteza malengo, inatakiwa
mchezaji alale mapema, akae kitandani awaze mechi ya kesho, ajiandae na mechi
kisaikolojia, lakini unapomuamsha usiku unamnyima muda wa kupumzika, pia
unamnyima nafasi ya kuuwaza mchezo wa kesho na matokeo yake analala na msongo
wa mawazo na hasira juu kutokana na kusumbuliwa usiku.
Matokeo
yake wanaingia kwenye mechi bila kuwa sawa kisaikolojia na wanafungwa si
kwasababu ya kukosa uwezo bali ni miundombinu ya viongozi kushindwa kuwaandaa wachezaji
kiuweledi.
Waganga
hawasaidii katika soka, maandalizi ya kitaalamu, kiuweledi ndiyo yanatoa nafasi
ya kupata matokeo. Simba na timu nyingine zote badilikeni!
Nawatakiwa
jumatatu njema, tukutane tena jumatano ya wiki hii!!





0 comments:
Post a Comment