Msuva (kushoto) na Tambwe (kulia) wakishangilia moja ya goli la Yanga msimu huu.
MFUNGAJI wa magoli 8 katika mechi tatu za Yanga, Mrundi
Amissi Tambwe amesema morali ya kutetea kiatu chake cha dhahabu imeongezeka
kutokana na mafanikio anayopata kwasasa.
Tambwe alifunga magoli manne (4) kwenye ushindi wa 8-0 dhidi
ya Coastal Union, akafunga goli moja (1) kwenye ushindi wa 3-2 dhidi ya Stand
United na mwishoni mwa juma lililopita alifunga magoli matatu (3) ‘hat-trick’
Yanga ikishinda 4-1 dhidi ya Polisi Morogoro.
Mfungaji huyo wa magoli 19 msimu uliopita anafukuziana na
mchezaji mwenzake wa Yanga, Simon Msuva kuwinda kiatu cha dhahabu.
Msuva ana magoli 17 , wakati Tambwe ana magoli 14 na
wamebakiwa na mechi mbili kumaliza msimu.
Tambwe ni mtu hatari wa kufumania nyavu licha ya kuzidiwa na
Msuva msimu huu na mechi zijazo tutarajie uchoyo kwa wachezaji hawa.
Inawezekana Tambwe akamnyima Msuva nafasi au kinyume chake.
Mechi iliyopita Msuva alifunga goli moja, lakini magoli
aliyofunga Tambwe yalichangiwa na Msuva ambaye alikuwa analazimisha kupiga,
kipa anatema halafu Tambwe kwakuwa anajua kujipanga anamalizia kiurahisi.
Kwahiyo Msuva ajiangalie kwasababu kama atakuwa analazimisha
kufunga, kipa anatema, basi Tambwe atakuwa mfungaji bora kutokana na ujanja
wake wa kukaa maeneo sahihi.
Lakini wachezaji hao wawili wanasemaje?
Tambwe: ‘Sasa hivi nimetulia, nina furaha Yanga, naweza
kutetea kiatu changu, niliachwa magoli mengi, sasa nimeachwa magoli matatu tu,
ninaweza kupindua kwa mechi mbili zijazo na kuchukua kiatu changu. Msuva
(Simon) ni mchezaji mwenzangu, nafurahia anavyofunga na kuisaidia timu, lakini
na mimi nahitaji heshima yangu, tutapambana tu. Kwanza ni jambo zuri wachezaji
wawili ndani ya timu moja kupambana namna hii”.
Msuva: “Namshukuru Mungu naendelea kufunga, najitahidi
kupambana ili kufunga zaidi ili wa nyuma yangu (Tambwe) asinikute, nakitaka
sana kiatu cha dhahabu”.
0 comments:
Post a Comment