AZAM FC imetamba kuzing’ang’ania pointi 9 zilizosalia katika
michezo yao mitatu iliyobakia kuhitimisha msimu huu wa ligi kuu soka Tanzania
bara.
Kocha msaidizi wa Azam, Dennis Kitambi amesema kufanya vibaya
kwao kumechangiwa na ratiba ngumu ya ligi kuu.
“Ulishawahi kuona wapi timu inacheza mechi nne za mashindano
ndani ya siku 11? Hakika ulikuwa mzigo kwetu kwasababu tulikuwa tunalazimika
kusafiri, mara Morogoro mara Tanga, tunarudi tena Dar. Ratiba haikututendea
haki”. Amesema Kitambi na kukiri; “Tumeshapoteza ubingwa wetu, lakini sasa
tunataka nafasi ya pili. Tuna hamu ya kukutana na Simba na Yanga, tunataka
kuchukua pointi zote ili kuchukua nafasi ya pili kwa kishindo”.
Mwishoni mwa juma hili Azam wenye pointi 45 baada ya kucheza
mechi 23 watachuana na Simba uwanja wa Taifa na mei 6 mwaka huu watakabiliana
na Yanga kabla ya kumaliza msimu kwa kuchuana na Mgambo JKT mei 9 mwaka huu.
Simba wanashika nafasi ya tatu kwa pointi 41
baada ya kucheza mechi 24 na wamebakiwa na mechi hiyo dhidi ya Azam na JKT
Ruvu, mechi zote zitapigwa uwanja wa Taifa
0 comments:
Post a Comment