WAKATI naifuatilia mechi ya jana ambayo Yanga walishinda 8-0 dhidi ya Coastal Union nilikaa na mashabiki wa Yanga ambao walikuwa wanasema timu yao ingeshinda zaidi magoli hayo kama si uchoyo wa Simon Msuva.
Msuva alifunga magoli mawili na kufikisha magoli 13 akizidi kukaa kileleni katika orodha ya wafungaji wa ligi kuu msimu huu akifuatiwa na Didier Kavumbagu wa Azam fc na Rashid Mandawa wenye magoli 10.
Kinara huyu wa magoli ana tatizo la kupiga pasi za mwisho na krosi. Ni jambo la kawaida kwa Msuva kufanya kazi kubwa, akawatoka mabeki na kuingia eneo zuri la kupiga krosi au pasi, lakini akalazimisha kupiga goli.
Amekuwa maarufu kupiga mashuti yasiyolenga lango bila sababu.
Jana alipata mipira mingi ambayo angetoa pasi kwa wenzake wangefunga, lakini yeye akawa analazimisha kupiga mashuti ili afunge mwenyewe.
Kuna wakati washambuliaji wanakuwa wachoyo, sehemu ya kutoa pasi kwa mwenzake mwenye nafasi nzuri zaidi anapiga mwenyewe, lengo linakuwa zuri kwani anahitaji kufunga, akikosa hapo ndipo atalaumiwa kwanini hakutoa pasi,akifunga watu wanasahau na kumpongeza.
Kutokana na baadhi ya watu kumlaumu, mtandao huu ukamfuata Msuva ili ajibu malalamiko haya.
"Kukosa goli ni sehemu ya mchezo, mimi ni mshambuliaji, kujaribu si kushindwa. Mimi sio mchoyo, kuna wakati unaweza kufikiri kwa haraka hapa nipige, moja ya kanuni ya kufunga ni maamuzi. Unaweza kumnyima mwenzako si kwa lengo baya, sema ukikosea kama ilivyonitokea mimi, lawama zitakuwepo".
"Kuna mengi mazuri tunafanya, hayo madogo madogo waachane nayo. Namshakuru Mungu timu inafanya vizuri na mimi nafunga. nitaendeleza juhudi zaidi". Amejibu Msuva.


0 comments:
Post a Comment