KIUNGO mkabaji wa Simba, Johans Gerrard Mkude amefiwa na baba yake mzazi, Mzee Gerrad Mkude aliyekuwa anasumbuliwa maradhi kwa muda mrefu kidogo.
Juzi akiwa hapa Shinyanga, Mkude alipigiwa simu kutoka nyumbani kwao Kinondoni, Dar es salaam kuwa baba yake kazidiwa na mpaka alipotangulia mbele ya haki.
Hili ni pigo kubwa kwa Mkude kwani baba yake bado alikuwa anahitaji kula matunda ya mwanae wa kumzaa aliyejaariwa kipaji kikubwa cha soka.
Mkude ni miongoni mwa wachezaji wa Simba waliopo mjini Shinyanga wakisubiri mechi ya kesho ya ligi kuu soka Tanzania bara baina ya Kagera Sugar na Simba, lakini yeye anaondoka leo kuelekea kumzika baba yake.
Kiongozi mmoja wa Simba aliyepo mkoani Shinyanga (hakupenda jina lake litajwe) amesema kuwa kwasasa Mkude yuko kambani mjini hapa na baada ya chakula cha mchana, ataondoka saa 7:00 mchana kuelekea jijini Mwanza kwa gari binafsi aina ya Noah.
Akifika Mwanza atapanda ndege saa 11:00 jioni kuelekea Dar es salaam tayari kwa shughuli ya mazishi.


0 comments:
Post a Comment