YANGA SC inahitaji ushindi au sare ya kuanzia 2-2 ili kusonga mbele katika michuano ya kombe la Shirikisho baada ya jana kutoka sare ya 1-1 na Etoile du Sahel kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya 16 bora.
Mechi ya marudiano itachezwa wiki mbili zijazo nchini Tunisia.
Benchi la ufundi la Yanga kupitia kwa kocha msaidizi, Boniface Mkwasa 'Master' limelalamikia ratiba ya ligi kuu kuwabana na kuwanyima muda wa kujiandaa katika michuano ya kimataifa.
"Ligi bado inatukaba, kama unavyojua ligi yetu haina mpangilio maalumu, mara leo unacheza, siku chache unacheza tena, kwahiyo utakuta majeruhi wanapatikana na inakuwa kama kero:, Amesema Mkwasa na kuongeza: "Tunaanza ligi jumanne (dhidi ya Stand United), nadhani wiki hii tutakuwa na mechi tatu za ligi na baada ya mechi ya mwisho itabidi tuondoke siku hiyo hiyo kwenda Tunisia".
Kocha huyo mzoefu amewashauri kitu TFF akisema: "Mimi nafikiri TFF kwa kipindi hiki wangeangalia namna ya kuipanga ratiba kwa timu inayoshiriki kombe la Shirikisho
Sasa unapocheza mechi nyingi unaweza kupata majeruhi wengine, matokeo yake inaathiri kiwango cha timu katika michuano ya kimataifa".
"Mfano jana tulimkosa Telela (Salum), kumbuka anacheza vizuri katikati na amekuwa na mchango mkubwa kwa timu, tulicheza mechi na Mbeya City na matokeo yake alipata majeruhi na hajafanya mazoezi, daktari alijitahidi kumpa matibabu lakini bado hakupona kwa haraka"
VIPI KUHUSU AMISSI TAMBWE?
Mkwasa ameeleza: "Tambwe (Amissi) jana alicheza hata kama alikuwa na marelia, lakini ikabidi tujaribu kumtazama kwasababu ya uzoefu wake ili aweze kuwasukuma wenzake kwani ana mchango mkubwa kwenye timu".
Yanga inaongoza katika msimamo wa ligi kuu ikiwa na pointi 46 baad aya kucheza mechi 21,ikifuatiwa na Azam wenye pointi 42 kwa mechi 22 walizocheza.

0 comments:
Post a Comment