KESHO ni usiku wa ligi ya mabingwa barani ulaya
ambapo mechi mbili za robo fainali zitashuhudiwa katika nchi za Hispania na
Italia.
Dimba la Vicente Calderon, wenyeji Atletico Madrid
watawakaribisha mahasimu wao wa mji, Real Madrid na mechi hiyo itachezeshwa na
muamuzi Milorad Mazic kutoka Serbia.
Huko Italia, Juventus watachuana na Monaco ya
Ufaransa, mechi zote mbili zitaanza majira ya saa tatu na dakika arobaini na tano kwa saa za Afrika
mashariki.
Atletico Madrid na Real Madrid zilizocheza fainali
ya ligi ya mabingwa mwaka jana na kesho zitakutana kwa mara ya saba msimu huu,
huku kila timu ikijipanga kulipa kisasi.
Mwezi mei mwaka jana mjini Lisbon, Ureno, Sergio
Ramos alizima ndoto za Atletico kutwaa ubingwa wa kwanza wa ulaya kufuatia
kusawazisha bao dakika za mwisho na kusababisha mechi ichezwe kwa dakika 120 na
ndipo Real wakashinda 4-1.
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa Atletico
wameshinda mechi nne na kutoka sare mbili katika mechi sita walizokutana msimu
huu.
Hii inajumuisha mechi mbili walizoshinda katika
michuano ya Kombe la ligi na kombe la Mfalme.
Hata hivyo mwezi februari mwaka huu, Real Madrid
walishushiwa kipigo cha mabao 4-0 katika mechi ya ligi kuu, La Liga na huo ulikuwa ushindi mkubwa zaidi kwa mechi za
mahasimu wa jiji la Madrid kwa miaka 28 iliyopita.


0 comments:
Post a Comment