Ushindi wa mabao 2-1 waliopata Azam fc dhidi ya Kagera Sugar katika mechi ya ligi kuu Tanzania bara iliyochezwa uwanja wa Azam Complex, Chamazi umewafanya wafikishe pointi 42 katika nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 22.
Mabao ya Azam yalifungwa na Frank Domayo na Gaudence Mwaikimba, wakati la kufutia machozi wa Kagera Sugar lilifungwa na Babu Ali Seif.
Hata hivyo goli la Mwaikimba lilizua mzozo baada ya wachezaji wa Kagera Sugar kumfuata mwamuzi wakidai mfunagji alikuwa ameotea.
Dhahiri Mwaikimba alikuwa ameotea wakati anapiga kichwa shuti la Brian Erick Majwega, lakini katika soka mwamuzi ndiye mtu wa mwisho kutoa maamuzi.
Baada ya mechi hiyo, nahodha wa Kagera Sugar, George Kavila alisema: “Mechi ilikuwa nzuri, tumecheza vizuri, lakini tumeumia sana kwa goli la Mwaikimba, mwamuzi msaidizi namba mbili anadai Mwaikimba hakugusa mpira, hivyo ni goli la Mwajwega, sio kweli, wote tumeona Mwaikimba akifunga kwa kichwa huku akiwa ameotea”
Kwa upande kocha wa Azam, George Best Nsimbe amekiri wazi kuwa Mwaikimba alifunga goli na ameotea, lakini hawana la kufanya, mwamuzi ameshaamua na wanashukuru kwa kuchukua pointi tatu.
“Hata sisi tuliona ameotea, lakini mwamuzi ndiye ana uamuzi wa mwisho, naangalia mechi ijayo na Stand United”
Yanga wanaendelea kushika nafasi ya kwanza kwa pointi 46 kwa mechi 21 walizocheza.
Mechi ijayo Azam watakabiliana na Stand United uwanja wa Azam Complex .


0 comments:
Post a Comment