STAND UNITED ikiwa uwanja wa nyumbani wa CCM Kambarage, Shinyanga, imeibamiza Mgambo Shootings ya Tanga mabao 4-1.
Taarifa kutoka Shinyanga zinaeleza kuwa Stand walikuwa kwenye ubora wa hali ya juu na kuwazidi kwa kila kitu maafande hao wa Jeshi la Kujenga Taifa.
Kutokana na ushindi huo Stand wamefikisha pointi 15 baada ya kushuka dimbani mara 15.
Mechi nyingi ya ligi kuu imepigwa uwanja wa CCM Nangwanda Sijaona Mkoani Mtwara ambapo wenyeji Ndanda fc waliwakaribisha Mtibwa Sugar.
Kipute hicho kilichokosa mvuto kutokana na soka bovu la timu zote kimemalizika kwa suluhu ya bila kufungana.
Nao Wagosi wa Kaya wameshindwa kutamba mbele ya Mbeya City fc baada ya kulazimisha suluhu ya bila kufungana uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga.
Hata hivyo dakika za usiku kipindi cha pili, Mbeya City walipata pigo baada ya Hamad Kibopile kuoneshwa kadi nyekundu.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi mbili kupigwa.
Polisi Morogoro wataikaribisha Simba SC uwanja wa Jamhuri Morogoro, wakati Kagera Sugar watachuana na JKT Ruvu uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.
0 comments:
Post a Comment