Wachezaji wa Friends Rangers wakitoka Uwanjani baada ya kuvunjika kwa pambano hilo dhidi ya Majimaji ya Songea.
Na Richard Bakana, Dar es salaam
Shirikisho la mpira wa miguu Nchini (TFF) kupitia kamati yake ya Utendaji na Usimamizi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania bara (TPLB) limeamua kuzipatia timu za Majimaji na Toto Afrika ushindi wa Pointi tatu na jumla ya mabao 3 kufatia michezo yao kunako ligi daraja la kwanza kuvunjika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam, Ofisa habari wa TFF, Bwana Baraka Kizuguto, amesema kuwa, kamati hiyo iliyokutana jana Februari 12, ikitumia Kanuni ya 28(4) ya FDL. ilipitia malalamiko ya Friends Rangers kwenye mechi dhidi ya Majimaji na kuamua kuyatupilia mbali huku timu hiyo ya Manzese ikisukumiziwa zigo la faini ya Tsh. 500,000 kwa kusababisha mchezo huo uliochezwa Januari 29 mwaka huu Uwanja wa Majimaji mjini Songea kuvunjika dakika ya 39.
Kizuguto amesema kuwa Friends Rangers imepoteza mechi hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 28(1) ya FDL,na Majimaji kutoka Songea wamekabidhiwa pointi tatu sambamba na magoli matatu.
Kwa upande wa Toto Africans, Kizuguto, amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 41(3) ya FDL, kamati imeipa ushindi timu hiyo baada ya vurugu za washabiki wa Geita Gold kusababisha mechi hiyo iliyochezwa Februari 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita kuvunjika dakika ya 12.
Mchezaji Venance Joseph wa Geita Gold ambaye alimpiga kichwa refa akipinga adhabu ya penalti iliyotolewa dhidi ya timu yake kwenye mechi hiyo amesimamishwa wakati akisubiri kosa lake kusikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mshambuliaji wa Geita Gold Sports Club, Kaicy Deo (Katikati) akiwa na wenzake.
Ili kuhakikisha ubabaishaji katika soka la Bongo unaisha, Kamati hiyo imeamua kumfungia Kamishna wa mechi hiyo Kim Rajab wa Dodoma kwa miezi 12 (kumi na mbili) kwa mujibu wa Kanuni ya 38(1) ya FDL kwa kutoa taarifa zisizo sahihi.
Naye Kocha wa Friends Rangers, Herry Chibakasa (Mzozo) suala lake limepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF ili aweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni ya 39(8) ya FDL kwa kuhamamisha vurugu kwenye mechi dhidi ya Majimaji.
Mwamuzi John Mafuru wa Mbeya aliyechezesha mechi ya Majimaji na Friends Rangers amefungiwa miezi 12 (kumi na mbili) kwa kutozingatia sheria kiasi cha kuvuruga mchezo. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 37(1) ya FDL.
Lipuli ya Iringa imepewa ushindi wa mabao matatu na pointi tatu baada ya timu ya KMC (Tessema) kumchezesha mchezaji Morris Paulo Katumbo aliyekuwa na kadi tatu za njano kinyume na Kanuni ya 41(12) ya FDL. Katumbo ambaye alipata kadi hizo kwenye mechi namba 85, 100 na 112 alicheza mchezo huo uliomalizika kwa timu ya KMC kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
0 comments:
Post a Comment