
DESEMBA 28, 2014, Nahodha wa Azam fc, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliifungia klabu yake bao la pili la kusawazisha na kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Dar Young Africans, mechi ya ligi kuu soka Tanzania bara uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Stori kubwa katika bao hilo ilikuwa kwamba, Bocco
alitokea benchi na mpira wake wa kwanza kugusa ndio alifunga goli hilo muhimu.
Bocco, mchezaji mwandamizi ndani ya kikosi cha Azam
amefanya kazi kama hiyo leo katika mechi ya ligi ya mabingwa barani Afrika
dhidi ya Al Merreick ya Sudan, Wanalambalamba wakishinda 2-0.
Bocco aliingia akitokea benchi akichukua nafasi ya
Kipre Herman Tchetche katika dakika ya 75’ kwenda 76’ na mpira wake wa kwanza
kugusa tu akafunga goli la pili dakika ya 77’.
Awali kipindi cha kwanza Didier Fortune Kavumbagu
aliifungia bao la kuongoza Azam fc katika dakika ya 8’.
Azam wanastahili pongezi kwa ushindi huo na sasa
wanajiandaa na mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki mbili zijazo nchini Sudan.
Al Merreick wanahitaji ushindi wa mabao 3-0 ili
kusonga mbele wakati Azam wanahitaji sare ya 1-1 au kufungwa bao 1-0 ili
kusonga mbele moja kwa moja.
Katika mechi ya leo, Azam wangeweza kufunga magoli
mengi endapo Salum Abubakar, Kipre Tchetche, Briam Majwega, Himid Mao Mkami
wangekuwa makini kwani walipata nafasi kadhaa za kufunga.
Kilichoonekana kuongezeka kwa Azam ni nidhamu
kubwa ya ulinzi hasa Pascal Wawa aliyehaha sehemu yote ya ulinzi kuhakikisha
hawafungwi goli.
Pia mlinda mlango Aish Manula, licha ya uchanga
wake amefanya kazi kubwa kulinda lango kwasababu aliokoa michomo ya mingi ya
hatari.
Lakini jambo la muhimu kwa kocha Joseph Marius
Omog ni kuhakikisha anaongeza nguvu kuwanoa washambuliaji wake kuelekea mechi
ya marudiano sambamba na kuwaongezea nidhamu ya kukaba katika sehemu zote za
uwanja.
Ushindi huu ni faraja kwa Watanzania kwani Yanga
nao walishindi 2-0 dhidi ya BDF XI ya Botswana katika mechi ya kwanza ya kombe
la Shirikisho barani Africa.

0 comments:
Post a Comment