Na Bertha Lumala, Dar s Salaam
Kikosi cha mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya Sudan, El-Merrikh kimetua jijini hapa leo mchana huku kikiichimba mkwara mzito Azam FC kuelekea mechi yao ya kwanza ya hatua ya awali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika itakayochezwa Uwanja wa Azam Jumapili.
Kikosi cha wachezaji 18 na viongozi kadhaa wa El-Merrikh kimewasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini hapa leo mchana na kwenda moja kwa moja Hoteli ya Serena jijini hapa.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Azam FC, Saad Kawemba, timu hiyo ya Sudan itafanya mazoezio kesho Uwanja wa Karume jijini hapa kabla ya keshokutwa kufanya mazoezi Uwanja wa Azam, Chamazi jijini.
Timu hiyo inayonolewa na Diego Garzito, ambaye amesema ana kikosi safi cha kuikalisha Azam FC Jumapili, hakina rekodi ya kutolewa mapema katika michuano ya kimataifa.
Kawemba amesema wanatarajia kuwa na mechi ngumu siku Jumapili dhidi ya timu hiyo kwani timu zote mbili zinafahamia vyema.
"Wageni wetu wameshawasili jijini Dar es Salaam tangu mchana, wamefikia Serena Hotel na kesho watafanya mazoezi Uwanja wa Karume. Viongozi wao wako nchini tangu juzi na jana walikuwa sehemu ya watazamaji walioshuhudia mechi yetu dhidi ya Mtibwa Sugar FC," amesema Kawemba.
El-Merreikh wanatamba na mshambuliaji wao hatari wa kimataifa Mkenya Allan Wanga.
Azam na El-Merrikh zilikutana kwa mara ya mwisho mwaka jana jijini Kigali, Rwanda katika robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Azam iking'olewa kwa mikwaju ya penalti.
0 comments:
Post a Comment