Baada ya kuondoka Yanga kwa mkopo sasa mambo yameanza kumnyokea mshambuliaji wa timu ya Polisi Morogoro, Said Bahanuzi kwa kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa mwezi Januari 2015.
Bahanuzi ambaye alikaa bench akiwa na Yanga kwa zaidi ya misimu wiwili sasa amekuwa ni mshambuliaji wa kutumainiwa kunako kikosi cha Polisi Moro na hatimaye leo amechaguliwa kunyakua tuzo hiyo ambayo kimsingi itamuinua sana na kumpa nguvu ya kufanya vyema zaidi katika ligi kuu ya Tanzania bara inayoendelea.
Mbali na Bahanuzi pia Kiungo wa timu ya Coastal Union, John Mahundi amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Disemba 2014 wa Ligi hiyo ambayo kwa ssa imefikia michezo ya 15 katika mzunguko wa pili.
Mahundi alitoa mchango mkubwa kwa timu yake ya Coastal Union mwezi Disemba mwaka jana na kuchaguliwa na jopo la makocha linalofanya kazi ya kuchagua mchezaji bora wa kila mwezi.
Kwa kuibuka wachezaji bora, Mahundi na Bahanuzi watazawadiwa fedha taslimu sh. milioni moja kwa kila mmoja kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.
Jopo maalumu la makocha waliopo katika viwanja vyote vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ndiyo wanaofanya kazi ya kuchagua mchezaji bora kwa kila mechi kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, na baadaye alama zao kujumlishwa ili kumpata mshindi wa mwezi.


0 comments:
Post a Comment